Habari Mseto

Majonzi ya mama aliyepoteza kifungua na kitinda mimba kwenye ajali

April 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na MERCY KOSKEI

FAMILIA moja ya Nakuru inaomboleza vifo vya kifungua na kitinda mimba waliongamia katika ajali ya barabarani iliyoangamiza watu saba eneo la Ngata, Jumanne asubuhi. Jumanne ilikuwa siku ya kawaida kwa Bi Selina Kemunto, ambaye hakutarajia habari za tanzia nzito.

Saa chache baadaye, mili ya wanawe wawili Godfrey Omwocha, 34, na kakake mdogo Jorum Atandi, 21, ilipelekwa katika mochari ya Nakuru Annex. Habari hizo za kushtua zilimfikia mjane huyo alipokuwa akiendelea na shughuli zake za kila siku.

Omwocha alikuwa dereva wa matatu ya kubeba abiria 14 ilhali nduguye mdogo alikuwa kondakta wa gari hilo.

Kaka hao walikuwa wakisafirisha abiria kati ya Nakuru na Kisii. Bi Kemunto alisema alifahamishwa kuhusu ajali hiyo na akakimbia mochari kutambua mili yao.

“Niliomba kimya kimya, siku hiyo. Nimepoteza wanangu wawili, walikuwa wachumia familia yangu riziki,” alisema.

Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binadamu linaitaka Serikali kuwafungulia mashtaka maafisa waliomuua Omar Faraj kimakosa wakati wa msako wa mshukiwa wa ugaidi mjini Mombasa zaidi ya miaka 12 iliyopita.

Muslims for Human Rights (Muhuri) imesema kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba polisi hawakutoa sababu halali ya kumpiga risasi Faraj ilithibitisha hakuwa na hatia.

“Tunataka maafisa wote wa polisi walioendesha msako huo wakamatwe na kufunguliwa mashtaka. Sheria lazima iruhusiwe kuchukua mkondo wake. Polisi hawakutoa maelezo kwa mahakama kuhusu sababu ya kumpiga Faraj risasi,” alisema mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Bw Khelef Khalifa.

Shirika hilo lilipongeza Mahakama Kuu kwa kuitunuku familia ya Faraj Sh6.5 milioni, baada ya kupata kwamba jamaa huyo aliuliwa kiholela kwani hakuna ushahidi uliowasilishwa kumhusisha na tuhuma zozote za ugaidi.

Muhuri ambayo iliishtaki Serikali na kushinda kesi hiyo, iliitaja hukumu ya Jaji Olga Sewe kama hatua muhimu katika uwajibikaji kwa ukiukaji wa haki za binadamu nchini Kenya.

“Ni mara ya kwanza kwa familia ya mwathiriwa kutunukiwa fidia kwa mauaji yanayohusiana na vita dhidi ya ugaidi,” Bw Khalifa alisema.
Bw Khalifa alisema vita dhidi ya ugaidi vimegeuka mara kwa mara kuwa umwagaji damu badala ya kutumia utaratibu unaostahili wa kisheria. Alisema mauaji ya Faraj ni moja tu ya visa vingi vya uhalifu unaofanywa na polisi kwa madai ya kupambana na visa vya ugaidi.

“Lakini lazima tukumbuke tuzo ya fedha haimrudishi Faraj kwa familia yake, wala haijawafanya waliohusika kuwajibikia makosa yao,” alisema.

Katika uamuzi wake, Jaji Sewe alisema Huduma ya Kitaifa ya Polisi haikutoa ushahidi wala kutoa maelezo yoyote kupinga madai kwamba mawakala wao, walihusika katika kumpiga risasi na kumuua Faraj bila sababu.

Jaji huyo alitegemea hati ya polisi ambayo ilisema kwamba Faraj, alipigwa risasi wakati wa mapambano kati ya polisi na mshukiwa wa ugaidi, wakati mshukiwa mmoja alikuwa ameenda kuwaonyesha polisi maficho yao (ya washukiwa wa ugaidi) katika eneo la Majengo.

Jaji Sewe alibaini kuwa maafisa waliohusika walitarajiwa kulinda eneo la tukio, kukusanya ushahidi, kuchunguza na kutoa taarifa kwa Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA), kuhusiana na tukio kama hilo ambapo utumizi wa bunduki ulisababisha kifo.

Kwa mujibu wa Jaji Sewe, polisi, kwa mfano, walipaswa kutoa ushahidi kwa njia ya OB au hati nyingine yoyote kama hiyo, ili kuonyesha kwamba Faraj alishukiwa kwa ugaidi au kwamba alikuwa na bunduki wakati wa tukio hilo.

Faraj ambaye alikuwa mhudumu wa duka la nyama, aliuawa kwa kupigwa risasi alfajiri ya Oktoba 28, 2012, wakati maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia kiraia walipovamia makazi yake.

Nyaraka za mahakama, zilifichua kuwa polisi kutoka kitengo cha kukabiliana na ugaidi walikuwa wanamsaka mshukiwa wa ugaidi Fuad Abubakar Manswab, wakati wa tukio hilo.

Faraj alikuwa akijaribu kutoroka kupitia dirishani wakati risasi ilipotua kwenye kichwa chake.

-Ripoti ya ziada na Brian Ocharo