Arsenal yapepetwa na Aston Villa
NA MWANGI MUIRURI
NI kilio na majonzi kwa mashabiki wa Arsenal huku wakishikilia kwamba ndovu angali juu ya mti baada ya timu kipenzi wanayoshabikia mnamo Jumapili, Aprili 14, 2024 kuadhibiwa na Aston Villa kwa mabao 2 – 0.
Magoli hayo yalifungwa ndani ya dakika tatu, la kwanza likitoka kwa guu la Leon Bailey katika dakika ya 84 na la pili likifuata kutoka kwa guu la Ollien Watkins katika dakika ya 87.
Mtanange huo wa 32 kwa Arsenal na wa 33 kwa Aston Villa kati ya yote 38, ulikuwa wa kuwania ubingwa wa ligi kuu ya Uingereza (EPL) na ulichezewa katika uga wa nyumbani wa Arsenal – Emirates
Timu ya Aston Villa hunolewa makali na kocha wa zamani wa Arsenal Bw Unai Emery, nayo Arsenal ikiwa mikononi mwa straika wake wa zamani, Mikel Arteta.
Arsenal ilishindwa kuchangamkia hali ya awali ambapo timu ya Liverpool ilikuwa imeshindwa kupaa hadi juu ya jedwali kwa kulimwa na timu ya Crystal Palace 1 – 0.
Kwa sasa, Manchester City ndiyo inaongoza jedwali kwa pointi 73, Arsenal ikifuata kwa pointi 71 sambamba na Liverpool ambayo pia ina pointi 71 lakini ikiwa na upungufu wa mabao.
Ushindi huo wa Aston Villa uliinyanyua hadi nafasi ya nne ikiwa na alama 63.
Arsenal ilimiliki mtanange huo kwa asilimia 52 dhidi ya 48 ya Aston Villa, ikipiga fataki 18 dhidi ya 11 lakini nne zikilenga kimyani bila bao lolote dhidi ya mbili za Aston Villa na zilizogeuka kuwa mabao.
Arsenal ilitandaza pasi 444 dhidi ya Aston Villa – 421 lakini hatimaye hali ikaishia ndovu kubakia katika matawi nayo Man City ikiwa juu ya mti.
Mkabano huo wa timu hizo tatu za kwanza katika jedwali bado una pointi zingine 18 za kung’ang’ania hadi mshindi abainike.