Mackenzie sasa hataona nje ya jela mpaka kesi dhidi yake ikamilike
MHUBIRI mwenye utata Paul Mackenzie na washtakiwa wenzake 94 wa vifo vya Shakahola watasalia gerezani hadi kesi ambayo wanakabiliwa na mashtaka 238 ya kuua bila kukusudia isikizwe na kuamuliwa.
Hii ni baada ya Mahakama ya Mombasa kukataa ombi la washukiwa hao kutaka kuwa huru huku wakisubiri kesi hiyo isikilizwe.
Hakimu Mkuu Alex Ithuku alitupilia mbali ombi la Bw Mackenzie na wenzake akisema kesi inayowakabili ina uzito mkubwa, na hawana mahali panapotambuliwa kuwa kwao kwa vile walikamatwa msituni Shakahola.
“Hakuna thibitisho kuwa washtakiwa wana makazi yanayojulikana kwa vile wote walikamatwa katika msitu wa Shakahola hivyo itakuwa vigumu kupatikana iwapo hawatafika mahakamani. Kwa hivyo itakuwa ni hatari kuwaachilia huru kwa dhamana,” alisema Bw Ithuku.
Kufikia sasa, serikali bado imefungia umma sehemu ya msitu wa Shakahola ambao umewekewa ulinzi mkali baada ya kuorodheshwa kuwa eneo la uhalifu.
Mahakama ilikubaliana na maelezo ya Idara ya Mashtaka ya Umma kuwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao yana uzito mkubwa hivyo basi wanaweza kutoweka au hata kuwaingilia mashahidi kwani wengi wao (mashahidi) ni watoto.
Pia, mashahidi hao walisememekana kuwa wengi wao ni waumini wa Kanisa la Mackenzie.
Bw Ithuku alieleza kuwa, washukiwa hao huenda wakakosa kufika kortini watakapopewa dhamana ikizingatiwa kuwa mashtaka yao yana adhabu ya kifungo cha maisha jela ikiwa watapatikana na hatia.
Hili, mahakama ilikubaliana na upande wa mashtaka, huenda likaweza kuwa sababu kuu washukiwa watoweke kabla ya kesi kusikizwa na kukamilika.
Upande wa mashtaka ulipinga majaribio yoyote ya kumwachilia Mackenzie na washukiwa wenzake kwa kwa hoja kwamba wanaweza kutoweka na pia kuwa hawana makazi maalum.
Pia, upande wa mashtaka ulidai kuwa Mackenzie na wenzake huenda wakaingilia mashahidi wakuu wakiwemo watoto na wahasiriwa wa mkasa huo ambao walikuwa waumini wa kanisa la Mackenzie.
Vilevile, mahakama iliambiwa kuwa Mackenzie amewahi kupatikana na hatia na kufungwa kwa makosa aliyofanya mwaka wa 2017 kabla ya kisa cha mwaka jana kuibuka.
Washukiwa hao wanashitakiwa kwa makosa 238 ya kuua bila kukusudia.
Wanadaiwa kutekeleza makubaliano ya kujitoa mhanga kwa lengo la kujiua na kuua watu 238 kwa pamoja.
Walidaiwa kutekeleza makosa hayo katika tarehe isiyojulikana kati ya Januari 2021 na Septemba 2023 katika eneo la Shakahola, Kaunti Ndogo ya Malindi.
Wote wamekana mashtaka yote ya kuua bila kukusudia. Kesi hiyo itatajwa Aprili 25.
Bw Mackenzie tayari anatumikia kifungo gerezani baada ya kupatikana na kosa la kusambaza filamu za itikadi kali katika kesi tofauti iliyokuwa ikimwandama.
Wiki chache zilizopita serikali ilianza kukabidhi miili iliyofukuliwa Shakahoa kwa familia mbalimbali ili kuandaa mazishi.
Hata hivyo ni miili 34 pekee iliyokuwa imetambuliwa kupitia kwa uchunguzi wa chembe za DNA.