Habari Mseto

Watoto wa bodaboda walivyonufaika na udhamini wa masomo

April 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

KAMPUNI ya kufadhili mali kwa njia ya mkopo ya Watu Credit, itafadhili masomo ya watoto ambao wazazi wao ni wahudumu wa bodaboda nchini.

Kwa sasa inafadhili masomo ya wamafunzi 37 kote nchini kwa kugharamia mahitaji yao kwa kipindi cha miaka minne.

Mpango huo uliozinduliwa 2022 ili kusaidia watoto wa waendesha bodaboda utalipa karo, kununua vitabu, sare za shule, kulipia nauli za usafiri ikiwemo pesa za mfukoni (Pocket money).

Meneja wa kampuni hiyo Bw Erick Massawe, alisema wanafunzi wanaonufaika ni kutokana na matokeo yao ya mtihani wa darasa la nane mwaka uliopita. Ufadhili huo pia, umempa mtoto wa kike kipao mbele haswa wale wanaotoka vijijini.

“Hawa ni watoto wa wateja wetu ambao wanatuthamini na nikutoka kaunti mbalimbali nchini. Ili kupata ufadhili huo ni kulingana na matokeo ya wazazi wao ambao wanabidii ya kulipa mkopo wetu kwa njia inayofaa,” alisema Bw Massawe.

Bw Massawe alisema mpango huo ulichochewa na wateja wao ambao wamekuwa nguzo muhimu kwa kukopa bidhaa kama vile pikipiki na Tuktuk ili kufanya biashara.

“Waendesha bodaboda ni nguzo muhimu ya jamii nchini ambao tunathamini kuwa wateja wetu. Tuliona ni vyema kuanza nao kwenye mpango huo kwa kuwa nguzo ya biashara yetu. Mpango huu ni fursa kwetu kusaidia kizazi kijacho cha viongozi katika jamii,” alisema Bw Massawe.

Tangu kuanzishwa programu hiyo, imenufaisha idadi ya wasichana 22 na wavulana 15, na kujitolea kuwekeza kwa viongozi wa siku za baadaye kwa kutoa ushauri na fursa za kujifunza.

Baadhi ya wanafunzi walionufaika na mradi huo, walisema kuwa waliweza kufadhiliwa masomo ya shule ya msingi kutokana na uchochole uliokuwa ukiandama wazazi wao ambao pia walichukua mkopo wa kuinua familia yao.

“Walilipa karo na wakati wa mikutano ya kitaaluma walikuwa wakija shuleni kuniona na kuzungumza nami,” alisema mwanafunzi mmoja.

Hata hivyo imeweza kuteua watumishi watakao dumisha mawasiliano na wanafunzi katika safari zao za masomo kupitia ziara za shule na nyumbani ili kufuatilia maendeleo yao na kutoa usaidizi zaidi.

Kampuni inasema imetoa mikopo ambayo imesaidia watu milioni nne ambao walikuwa wameathrika kimaisha.