Mwana aahidi jamii miradi sawa na babake Ogolla
NA BENSON MATHEKA
MWANAWE Jenerali Francis Ogolla, Joel Rabuku, ameahidi kuendelea na moyo wa baba yake wa kusaidia jamii kwa kukarabati taasisi za masomo katika Kaunti ya Siaya.
Alisema kwamba baba yake alikuwa akisaidia jamii kwa miradi ya maendeleo hata zaidi ya wanasiasa wanaopenda kutoa ahadi na kukosa kutimiza na kwamba atamuiga na kuendelea kufanya hivyo.
“Alikuwa na mpango kabambe wa kukarabati shule mnazoona katika eneo hili katika muda wa miaka miwili au mitatu. Si lazima uwe mwanasiasa ili ulete mabadiliko nchini. Wakati mwingine wanasiasa huwa wanapiga kelele lakini hatuoni matokeo na siogopi kusema hivyo. Ninachoomba ni muendelee kuniunga mkono. Nitabadilisha eneo hili,” alisema Bw Rabuku akihutubia waombolezaji waliohudhuria ibada ya wafu ya baba yake katika uwanja wa shule ya sekondari ya seneta Barack Obama, Ng’iya, Kaunti ya Siaya.
Marehemu Jenerali Ogolla atakumbuka kwa kusaidia wakazi wa kijiji cha Mor, Siaya kwa miradi ya maji na hata kujenga shule na makanisa.
Bintiye Jenerali Ogolla, Lorna, alisema baba yake hakuwa mtu wa kushindwa na chochote alichopania kufanya au kujukumiwa kufanya kibinafsi na kazini.