Habari Mseto

Jinsi usalama ungali donda ndugu kwa wanahabari wanaofuatilia habari za ulanguzi wa wanyamapori

April 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

WAHARIRI nchini wamehimizwa kuwasaidia wanahabari ili kuboresha uanahabari unaoangazia ulanguzi wa wanyamapori na uhalifu wa kimazigira katika eneo hili.

Haya ni kulingana na Bi Rosalia Omungo, Afisa Mkuu mtendaji wa Chama cha wahariri nchini, ambaye alikuwa akizungumza wakati wa majadiliano yaliyoandaliwa na shirika la Internews Earth Journalism Network, jijini Nairobi.

Aidha, Bi Omungo alisema kwamba wahariri wanapaswa kuhamasishwa zaidi kuhusu uanahabari kuhusu mabadiliko ya tabianchi na uhalifu wa kimazingira, ili kushinikiza wahusika kuwajibika.

Uhalifu wa kimazingira ni tatizo kuu eneo la Afrika Mashariki, na japo ripoti zinaonyesha kwamba eneo hili limepiga hatua katika nyanja hii, bado tatizo hili limezidi kuwa  donda sugu.

Kulingana na wataalam, mojawapo ya sababu ambazo zimeendeleza shida hii ni mada hii kutoangaziwa vilivyo na vyombo vya habari.

“Eneo la Afrika Mashariki lingali nyuma katika masuala ya uanahabari wa masuala haya kwa sababu ya uhaba wa rasilimali za kuwasaidia wanahabari kufuatilia habari hizi,” alisema Bi Omunga.

Wanahabari na wahariri katika picha ya pamoja wakati wa mafunzo ya uanahabari unaoangazia ulanguzi wa wanyamapori na uhalifu wa kimazigira Afrika Mashariki. Picha|Hisani

Akizungumza kwa njia ya mtandao, Bi Amanda Gore, mshauri wa upelelezi wa masuala ya kifedha katika shirika la EJN na mkurugenzi wa shirika la Centre for Global Advancement (C4GA), pia alitaja tatizo la ufikiaji taarifa muhimu, kuwa kizingiti kikuu katika uanahabari wa kuangazia uhalifu wa kimazingira katika eneo hili.

“Japo ni rahisi kupata taarifa unapowahoji watu eneo hili, changamoto kuu ni kufikia taarifa na ripoti katika taasisi. Hii ni tofauti pengine ukiangazia bara la Asia ambapo japo ni ngumu kuwahoji raia, kwa upande mwingine, taarifa nyingi zimenakiliwa, na hivyo unaweza kuzifikia,” aliongeza.

Hata hivyo, changamoto kubwa hata zaidi katika uanahabari unaoangazia ulanguzi wa wanyamapori na uhalifu wa kimazingira katika eneo hili, ni usalama wa wanahabari. Lakini hili sio tatizo la Afrika Mashariki tu. Ni shida duniani kote.

Kulingana na kamati ya kuwalinda wanahabari New York-based Committee to Protect Journalists (CPJ), kati ya mwaka wa 2009 na 2021, takriban wanahabari 30 wa kimazingira, waliuawa kutokana na kazi zao.

Kulingana na Bw Victor Bwire, Naibu afisa Mkuu Mtendaji na Msimamizi wa Mipango katika Baraza la Vyombo vya Babari nchini MCK, kutokana na haya, vyombo vya habari vinapaswa kubuni njia za kuangazia masuala haya, huku kwa wakati huo huo vikipunguza hatari ya usalama wa wanahabari.

“Kwa mfano, ni wakati wa kushirikiana na wanahabari kutoka nchi zingine na makala ya aina hiyo kuchapishwa na wanahabari kutoka nchi zingine,” aliongoza.

Mjadala huu ulikuwa sehemu ya mradi wa Following the Money wa shirika la EJN, ambapo wanahabari 12 kutoka Kenya, Tanzania, Uganda, Sudan Kusini na Rwanda walichaguliwa na wanaendelea kupokea mafunzo, ambapo wanatarajiwa kuandika habari za kupeleleza ulanguzi wa wanyamapori na uhalifu wa kimazingira. Watafanya hivyo kwa ushirikiano na wanahabari kutoka bara la Asia.

[email protected]