Watu 10 wafariki Malaysia kufuatia ajali ya helikopta mbili
NA MASHIRIKA
KUALA LUMPUR, MALAYSIA
WATU 10 wameaga dunia baada ya helikopta mbili kugongana hewani wakati wa maandalizi ya hafla moja ya Jeshi la Wanamaji la Malaysia, jeshi hilo limesema kwenye taarifa.
Ajali hiyo ilitokea katika kambi ya jeshi hilo la wanamaji iliyoko katika jimbo la Perak, magharibi mwa Malaysia mwendo wa saa tatu na dakika 32 za asubuhi.
“Wahanga wote walithibitishwa kufa katika eneo la tukio na maiti zao zikapelekwa katika hospitali ya kambi ya kijeshi ya Lumut ili zitambuliwe,” jeshi hilo la wanamaji lilisema.
Helikopta moja aina ya Agusta Westland AW139 ilianguka karibu na uwanja wa michezo ilhali ya pili aina ya Eurocopter Fennec ilianguka karibu na kidimbwi cha kuogelea.