Wakulima wa kahawa wapata faida mnadani
WAKULIMA wa kahawa wanaoshirikiana na vyama mbalimbali vya ushirika wamepata Sh1.058 bilioni katika soko la upigaji mnada kahawa na ubadilishanaji wa fedha la Nairobi (NCE).
Kiasi hicho cha fedha kilikuwa cha juu ikilinganishwa na Sh802 milioni zilizopatikana wiki jana kutoka kwa magunia 19,804 yaliyouzwa.
Wiki hii, magunia 26, 449 yaliyochukuliwa kutoka kwa vyama vya ushirika 1, 081 kote nchini yaliuzwa.Katika mnada huo jumla ya magunia 5,056 ya daraja la AA yaliuzwa na kufanya jumla ya pesa zilizopatikana kuwa Sh247.6 milioni kutoka kwa wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.Magunia 10, 377 ya daraja la AB yaliwapa wakulima Sh433.98 milioni.
Alliance Berries Ltd iliongoza mawakala wengine wa kahawa kwa kuuza magunia 7,546 kwa Sh328.764 milioni ikifuatiwa na Kirinyaga Slopes Ltd iliyouza magunia 7,371 ya kahawa kwa Sh264.58 milioni.
New Kenya Planters Cooperative Union (NKPCU) iliibuka ya tatu kwa kuuza magunia 4,739 kwa Sh212.89 milioni.
Miongoni mwa magunia yaliyouzwa na NKPCU, magunia 1,248 yalikuwa ya daraja la AA ambayo yaliingiza Sh64.301 milioni.
Miongoni mwa viwanda vya kahawa vilivyofanya mauzo ya juu ni kiwanda cha Konyu cha Kirinyaga kilichouza magunia 43 ya daraja la AA na kupata Sh8.169 milioni.
Viwanda vya Guama na Gaturiri viliuza jumla ya magunia 81 ya daraja la AA na kupata Sh7.577 milioni.
Kiwanda cha kahawa cha Karatina kupitia Alliance Berries Limited pia kiliuza magunia 133 ya AA kila moja kwa Sh60,702 kwa gunia.
Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa NCE, Lisper Ndungu, alisema katika wiki chache zilizopita kuwa bei ya kahawa imepanda jambo ambalo limewafanya wakulima kupata faida.
Alisema wanunuzi 19 wa ndani na nje wamevutiwa na kahawa na kuongeza kuwa wanunuzi wanavutiwa sana na ubora wa kahawa inayouzwa NCE.Viwanda vinne vikiwemo Konyu, Guama, Gaturiri na Karatina, viliwasilisha kahawa ya hali ya juu ambayo iliuzwa kwa bei ya juu.
Afisa huyo aliyezungumza na KNA kwa njia ya simu alisema viwanda vingine ambavyo kahawa yao ilifikia Sh53,000 kwa gunia ni pamoja na Ndaroini, Kagumo, Iyego na Mukengeria.
Katika kitengo cha wanunuzi wa kahawa, afisa Ndung’u alieleza kuwa Ibero Kenya ilinunua magunia 5,960 kwa Sh264.58 milioni, ikifuatwa na C.Dorman Ltd iliyonunua magunia 4,308 kwa Sh222.27 milioni.
“Wanunuzi wengine walikuwa Kenyacof magunia 5,622 kwa Sh213.66 milioni, Louis Dreyfus magunia 5,511 kwa Sh198.89 milioni, wafanyabiashara wa kahawa wa Jowam walinunua magunia 1,163 kwa Sh42.9 milioni,” alisema afisa huyo wa NCE.