Habari Mseto

Thiwasco yaimarisha mazingira kwa upanzi wa miti

April 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya maji mjini Thika (Thiwasco) inaendelea na mpango wake wa kila mwaka wa upanzi wa miti kuimarisha mazingira.

Mnamo Ijumaa wiki jana, wafanyakazi wa kampuni hiyo walipanda miche 5,000 katika kituo chao cha kusafisha maji machafu cha Kang’oki mjini Thika.

Mwenyekiti wa Thiwasco Bw Joseph Wakimani alisema kampuni hiyo ilianzisha mpango huo wa upanzi wa miti mnamo 2019 na tangu wakati huo inahakikisha hilo linafanyika kila mwaka.

“Hata mwaka 2023 tulipanda miti 5,000 na tutazidi kuendeleza mpango huo kila mwaka,” akasema mwenyekiti huyo.

Bw Wakimani alisema mpango huo unaendeshwa kwa ushirikiano na washika dau wengine mjini Thika kama kampuni ya Kel Chemicals, Thika Cloth Mills, vyuo vikuu kama Mount Kenya (MKU), shule za msingi mjini Thika na wafanyabiashara wanaotaka kuboresha mazingira ya Thika.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika Bw Alfred Wanyoike alipongeza juhudi za kampuni ya Thiwasco za kupanda miti mjini Thika ili kubadilisha mazingira.

Alisema huku mji wa Thika ukitarajiwa kugeuzwa jiji, ni bora kuwe na mazingira mazuri.

“Tunataka kuona mji wa Thika ukirejelea ubora wake na sifa ya usafi jinsi ilivyoshuhudiwa miaka za themanini (1980s),” alisema Bw Wanyoike.

Alitoa wito kwa washikadau wote popote walipo kufanya juhudi kuona ya kwamba mji wa Thika unapata mazingira ya kupendeza hasa katikati mwa mji na vitongoji vyake.

Alisema wakati huu ambapo mvua inanyesha katika maeneo mengi nchini, “ni vyema kila mmoja wetu kuchukua jukumu na kupanda angalau mti mmoja ili kulinda mazingira yetu”.