Watu 155 waaga dunia TZ kufuatia mafuriko, maporomoko ya ardhi
NA MASHIRIKA
DAR ES SALAM, TANZANIA
WATU 155 wamepoteza maisha na wengine 236 kujeruhiwa kufuatia mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini Tanzania, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa amesema.
Majaliwa aliliambia Bunge la Tanzania kwamba mafuriko hayo yanayosababishwa na mvua ya El Nino inayoshuhudiwa katika ukanda wa Afrika Mashariki pia yameharibu barabara, madaraja na reli.
“Mvua kubwa ya El Nino ikiandamana na upepo mkali, mafuriko na maporomoko ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini imesababisha uharibifu mkubwa,” Majaliwa akawaambia wabunge mnamo Alhamisi jioni.
Mvua ya El Nino husabibishwa na mabadiliko ya hali ya anga yanayochangiwa na ongezeko la joto duniani baada ya kipindi kirefu cha kiangazi.
“Madhara yaliyosababishwa na mvua hiyo kimsingi, yalichochewa na uharibifu wa kimazingira, shughuli zisizofaa za kilimo na mienendo mibaya ya kulisha mifugo,” akaongeza.
Waziri huyo Mkuu alieleza kuwa zaidi ya watu 200,000 na familia 51,000 zimeathiriwa na mvua hiyo.
Shule zilizoathiriwa na mafuriko zilifungwa na wahudumu wa mashirika ya uokoaji walikuwa wakiwaokoa wale ambao makazi yao yalizingirwa na maji.
Majaliwa aliwaonya watu wanaoishi katika maeneo ya nyanda za chini kuhamia katika maeneo ya miinuko.
Aidha, alitoa wito kwa maafisa wa serikali katika ngazi za wilaya kuhakikisha watu ambao makazi yao yalisombwa na maji wanagawiwa chakula na mahitaji mengine ya kimsingi.
Kufikia Aprili 14, 2024, serikali ya Tanzania ilisema kuwa jumla ya watu 58 wakiwemo watoto, walikuwa wameuawa katika mafuriko kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu Aprili.
Nchi nyingine za Afrika Mashariki kama vile Kenya na Burundi pia zimeathirika na uharibifu unaosababishwa na mvua kubwa.