Habari MsetoHabari za Kitaifa

Shule zilizoathiriwa na mafuriko kusalia kufungwa, Serikali yasema

April 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

Na WAANDISHI WETU

SHULE zilizoathirika na mafuriko hazitafunguliwa leo Jumatatu, Aprili 29, 2024 kwa Muhula wa Pili baada ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha sehemu mbali mbali nchini kusababisha hasara na vifo vya zaidi ya watu 70 na kuacha wengine 14,000 bila makao.

Hii ni baada ya Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ikiongozwa na Mkurugenzi Dkt David Gikungu kuonya kuwa mvua hiyo itaendelea tena kwa siku saba huku maporomoko ya ardhi yakitarajiwa sehemu kadhaa.

Hata hivyo, serikali imechukua hatua ya kufungua shule ambazo hazijaathiriwa na mafuriko.

Waziri wa Elimu Bw Ezekiel Machogu aliiambia Taifa Leo kwa njia ya simu kuwa shule zitafunguliwa hii leo kama ilivyopangwa kulingana na kalenda ya elimu.

“Hata hivyo, shule zilizoathirika na mafuriko hazitafunguliwa leo kutoka likizo,” alisema Bw Machogu.

Haya yanajiri huku mvua ikiendelea kunyesha na mabwawa kama lile la Masinga na Thiba yakitarajiwa kufurika baada ya maji kujaa pomoni.

Hii huenda ikaathiri kaunti ya Tana River ambapo maji hayo humwagika yakielekea Bahari Hindi.

Muungano wa Kitaifa wa Wazazi ukiongozwa na mwenyekiti wake Bw Silas Obuhatsa, umepongeza uamuzi wa serikali wa kutoahirisha kufunguliwa kwa shule isipokuwa zile ambazo zimeathirika.

Bw Obuhatsa alisema Wakenya hasa wanafunzi na walimu waliteseka sana wakati serikali ilipofunga taasisi zote za elimu nchini kutokana na janga la Covid-19 kwa zaidi ya miezi saba.

Bw Obuhatsa alisema serikali haiwezi kuahirisha ufunguzi wa shule zote nchini sababu sio kote kuna mafuriko.

“Itakuwa ni hujuma kuamua kuahirisha ufunguzi wa shule zote za umma ilhali sehemu zengine kama Mombasa hazijakumbwa na mafuriko ndio maana serikali imetoa uamuzi huo wa kutathmini zile ambazo zimeathirika. Isitoshe, tulijifunza mengi kutokana na janga la Covid-19,” aliongeza.

Alisema wanafunzi na walimu walishindwa kumaliza silabasi na hivyo basi kuandikisha matokeo duni ya mitihani ya kitaifa ya darasa la nane na kidato cha nne.

Hata hivyo, aliisihi serikali kuhakikisha usalama wa watoto hasa sehemu zinazoendelea kukabiliana na mafuriko.

“Watoto wapelekwe sehemu salama, hasa sehemu za Tana River na Kisumu ambazo zina historia ya majanga ya mafuriko. Kuna shule tayari zimezama sababu ya mafuriko, naomba wazazi tuwe watulivu, usalama wa watoto na walimu wetu ni muhimu zaidi,” aliongeza.

Naye waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen, amewataka wazazi na madereva kuwa waangalifu wakati huu wanafunzi wanaporudi shuleni. Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Bw Murkomen alisema mvua kubwa imeharibu barabara, kufanya mito kufurika na madereva wanapaswa kuwa waangalifu.

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha imeathiri uchukuzi wa ndege huku Shirika la Ndege la Kenya (KQ) Jumamosi usiku likielekeza safari za ndege katika viwanja vingine vya ndege kutokana na mvua kubwa iliyotatiza ndege kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Katika taarifa, shirika hilo la kitaifa pia lilionya kuhusu kucheleweshwa kwa safari za JKIA kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Jumamosi usiku na kusababisha marubani kutatizika kutua.

“Kutokana na mvua kubwa na kutoweza kuona vizuri jijini Nairobi, tumebadilisha safari zetu za ndege, jambo ambalo linaweza kusababisha kuchelewa kwa baadhi ya safari zetu kutoka Nairobi,” KQ ilisema.

Shirika hilo la ndege liliomba radhi kwa usumbufu uliotokea lakini likasisitiza kuwa usalama wa wateja na ndege unasalia kuwa kipaumbele.

Naye Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru ametangaza hatua za dharura za kukabiliana na mafuriko na hatari zingine zinazotokana na mvua kubwa katika kaunti hiyo.

Waiguru pia aliwaomba watu wanaoishi karibu na Bwawa la Thiba na maeneo ya chini ya mto kuwa waangalifu kwa sababu bwawa hilo linajaa maji kwa haraka sana.

Kuna hofu kwamba bwawa hilo linaweza kupasuka kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.

Alisema kamati ya ufuatiliaji wa maafa imeundwa ili kufuatilia kwa makini hali hiyo na kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea pamoja na kuchukua hatua za haraka panapohitajika.

Katika Kaunti ya Murang’a, Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA) imeagiza kamati ya usalama ya kaunti hiyo kusimamisha shughuli katika matimbo ya mawe, changarawe na mchanga kufuatia mvua kubwa inayoyaweka katika hatari ya kuporomoka.

Kupitia barua kwa kamati hiyo ya usalama, machifu, manaibu wao na wanachama wa Nyumba Kumi, Mkurugenzi wa NEMA Sarah Waruo, alisema kusimamishwa kwa shughuli katika machimbo hayo kutaokoa maisha ya wachimbaji wanaohudumu katika maeneo hayo.

Katika wiki ya pili ya Aprili, timbo moja katika eneo la Maragi liliporomoka na kujeruhi wachimbaji wawili.

RIPOTI ZA WINNIE ATIENO, HILLARY KIMUYU, GEORGE MUNENE, GEORGE ODIWOUR NA KNA