Maelfu hatarini kupoteza ardhi Portland kwa kukosa kuhalalisha umiliki
NA STANLEY NGOTHO
MAMIA ya maskwota wanaoishi katika Kampuni ya East African Portland (EAPCC) katika Kaunti Ndogo ya Mavoko iliyoko Machakos, wanakabiliwa na hatari ya kufurushwa kutoka kwa ardhi hiyo baada ya kukosa kuhalalisha mashamba yao.
Kampuni hiyo ya saruji sasa iko mbioni kuuza ploti 2,872 ambazo hazijasajiliwa miezi sita baada ya mchakato wa kuhalalisha kuanza.
Mnamo Oktoba 17, 2023, EAPCC ilitoa notisi ya siku 14 kwa umma kupitia magazeti ya kila siku kuuza sehemu ya ardhi LR No 8784/144,145 na 653 yenye ukubwa wa ekari 709 chini ya mfumo wa kuhalalisha.
Wanaomiliki sehemu za ardhi walipaswa kupewa kipaumbele.
Hata hivyo, asilimia kubwa ya wamiliki wa ploti wameshindwa kuzisajili na hivyo kusababisha EAPCC kwa ushirikiano na Geoner Consultant, kupitia ilani katika magazeti, kutangaza kuuza ploti hizo ambazo hazijahalalishwa.
Katika muda wa majuma mawili, wataalamu wa upimaji ardhi, wakiandamana na maafisa wa polisi waliojihami, wamekuwa katika ardhi hiyo wakitambua ploti ambazo hazijasajiliwa.
Wananchi wamealikwa kutuma maombi ya kununua takriban ploti 2,872 zenye ukubwa wa futi 40×80, 50×100. Zabuni itafungwa Mei 2.
Afisa wa cheo cha juu wa Eapcc ambaye hakutaka kutajwa jina aliambia Taifa Leo kwamba baada ya ploti zitakazotambuliwa kuuzwa, wanaozimiliki kwa sasa watatakiwa kuhama au watimuliwe.