Habari Mseto

Mkuu wa Bomas afunguliwa mashtaka

April 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA Mkuu Mtendaji wa Bomas of Kenya (BoK) ameshtakiwa kwa kununua vijiko, vikombe na vifaa vya jikoni bila mpango.

Bw Peter Gitaa Koria alishtakiwa mbele ya Hakimu Mkuu wa mahakama ya kesi za ufisadi, Thomas Nzioki. Alidaiwa kukaidi kifungu cha sheria za ununuzi katika mashirika na idara za serikali nambari 44 (2) (a) ya mwaka wa 2015.

Bw Koria anayewakilishwa na mawakili Dkt Ken Nyaundi, Danstan Omari na Bryan Khaemba, alikabiliwa na mashtaka saba ya kuvunja sheria za ununuzi wa bidhaa za kutumika katika mashirika ya umma kama vile BoK.

Hata hivyo, alikana kukaidi sheria hiyo kati ya Juni 30, 2020 na Juni 30, 2021.

Mahakama ilielezwa ununuzi huo ulifanywa bila ya kuwekwa katika bajeti ya mwaka wa matumizi ya pesa za umma. Korti ilifahamishwa kuwa matumizi hayo hayakuidhinishwa na kamati husika.

Kinara huyo wa BoK alidai kushtakiwa kwake ni kuonewa kwa vile hakuna ushahidi unaomlenga hata kidogo.

Upande wa mashtaka haukupinga mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana. Akitoa uamuzi kuhusu ombi hilo, Bw Nzioki alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh5 milioni au alipe dhamana ya pesa taslimu Sh1milioni.

Kesi hii itatajwa Mei 9,2024 kwa maagizo zaidi.