Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta atoa Sh2 milioni kusaidia waathiriwa wa mafuriko
NA LABAAN SHABAAN
ALIYEKUWA Rais Uhuru Kenyatta ametoa mchango wa kibinafsi wa Sh2 milioni kwa waathiriwa wa mafuriko nchini.
Fedha hizo zitapokewa na shirika la kutoa misaada la Red Cross katika hazina ya kusaidia waliovurugwa na mafuriko.
“Kama taifa, lazima tusimame pamoja tunapokabiliwa na changamoto, kudhihirisha upendo, uvumilivu, na kuishi kwa umoja na kushirikiana,” Rais wa awali alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Akisikitishwa na athari mbovu ya mvua kubwa inayoponda nchi, Bw Kenyatta alituma risala za rambirambi kwa walioathiriwa.
“Kwa nia ya huruma na kusaidia, Kenyatta amependekeza mchango wa kibinafsi wa Sh2 milioni kwa Shirika la Red Cross. Ni msaada unaolenga kuzidisha juhudi za msaada na kutoa bidhaa muhimu kwa familia zilizoathiriwa,” Rais wa awali alisema.
Mvua kubwa inayoendelea kunyesha imeathiri Nakuru, Nairobi, Homa-Bay, Garissa, Kisumu, Mombasa, na maeneo kadhaa ya Kati, Mashariki, na kaunti za Bonde la Ufa.
Takwimu za hivi punde kutoka kwa Wizara ya Usalama zinaonesha kuwa watu 169 wamefariki kutokana na mafuriko huku 102 wakijeruhiwa.
Wengine 91 hawajulikani waliko katika kipindi ambacho familia 30,099 zimefurushwa makwao makazi yaliposombwa na maji. Kufikia sasa, takriban watu laki mbili wameathiriwa na mafuriko.
Bw Kenyatta aliomba Wakenya wote waungane ili kusaidia kukabili changamoto za mafuriko akiomba madaktari wa kujitolea wasaidie walioathiriwa.
Kuhusiana na changamoto zinazoathiri sekta ya afya madaktari wanapoendelea na mgomo, Bw Kenyatta amesisitiza umuhimu wa mashauriano yanayoweza kuzaa matunda.