Habari Mseto

Mwanamke mjamzito kati ya walionusurika mauti kimiujiza Mai Mahiu

May 1st, 2024 2 min read

JOSEPH OPENDA NA MERCY KOSKEI

MWANAMKE mjamzito anayetarajiwa kujifungua wiki mbili zijazo ni kati ya waliookolewa kwenye mafuriko yaliyoathiri wakazi wengi Mai Mahiu mnamo Jumatatu usiku.

Kwa mujibu wa mkazi wa kijiji cha Sagre, Simon Mwangi, 29, ambaye ni kati ya manusura, mkewe mjamzito alinusurika kimiujiza janga hilo lililosababisha mauti ya watu 52.

Kabla ya tukio hilo, familia ya Bw Mwangi ilikuwa ikijiandaa kumkaribisha mtoto mwingine na hata alikuwa amemwaalika dadake mkewe aishi nao wakijiandaa kumpata mtoto huyo.

Supritendanti wa Hospitali ya Naivasha, Dkt Bernard Warui, alisema kuwa mkewe Bw Mwangi anaendelea kupata afueni na yupo katika hali nzuri kiafya. “Yuko salama na tunamwaangalia kwa makini ili kusitokee tatizo lolote,” akasema Dkt Warui.

Bw Mwangi na wanafamilia wake watano waliokolewa kisha kukimbizwa hospitalini pamoja na manusura wengine.

“Kila dakika namwombea mke wangu na mtoto wetu ambaye hajazaliwa. Kwa kuwa tumepitia machungu sana, naomba ajifungue salama,” akasema akiwa amelazwa hospitalini.

Katika umri huo mdogo, Bw Mwangi alikuwa amejenga nyumba ya aushi kwenye kipande cha ardhi alichonunua miaka mitatu iliyopita katika kijiji hicho.

Mafuriko hayo yamemrejesha nyuma kwa kuwa alikuwa amejitahidi kujenga nyumba hiyo kutokana na kazi yake ya uchukuzi wa bodaboda.

Bw Mwangi anakadiria kuwa amepoteza mali ya zaidi ya Sh2 milioni kutokana na mafuriko hayo. Mafuriko hayo pia yaliathiri vijiji vingine vitatu Mai Mahiu.

Wakati wa mahojiano, Bw Mwangi alisema kuwa mafuriko hayo ya kushtukiza yalimpata akiwa amelala pamoja na mkewe na watoto wake.

“Kabla tuondoke kitandani, maji yalikuwa yashatufikia na ukuta moja wa nyumba ulikuwa umeporomoka. Niliangukia matofali kabla ya paa kuniangukia na nikasombwa,” akasema Bw Mwangi.

“Sikumwona mke wangu, watoto na jamaa wengine. Niligongwa na mabati na miti ila nikashikilia nyanya ya ua kisha nikaitisha msaada,” akaongeza.

Mwili wake ukiwa umekatwa na kukwaruzwa, alipata fahamu hospitalini baada ya kupokezwa matibabu maalum.

“Namshukuru Mungu kuwa nipo hai pamoja na jamaa zangu. Najua watu wengi wamepoteza maisha yao na hilo ni jambo la kusikitisha mno,” akasema Bw Mwangi.

Licha ya kupoteza pikipiki yake, mifugo na samani ya nyumba, Bw Mwangi anashukuru kuwa yupo hai.

“Nilikuwa nimepanga kujenga choo na pia nilikuwa naweka akiba ya kujenga nyumba nyingine. Hata nilikuwa nishanunua vifaa na nilikuwa najibidishe nidundulize pesa za kuwalipa wafanyakazi. Sasa kila kitu kimeharibika na nitayaanza maisha mapya,” akasema.