Rais aagiza NCPB ifungue malango yake wahanga wa mafuriko wapate chakula
NA RICHARD MAOSI
RAIS William Ruto ameamuru Wizara ya Kilimo, kupitia Bodi ya Kitaifa ya Mazao na Nafaka Nchini (NCPB) kusaidia katika uwasilishaji na usambazaji wa chakula kwa waathiriwa wa mafuriko.
Alisema serikali inashirikiana na washikadau kutoa makao ya muda na mahitaji mengine ya kimsingi wakati huu nchi inapokumbwa na mvua kubwa na hatari ya mafuriko.
“Kwa sababu ya mvua nyingi inayoendelea kushuhudiwa nchini watu wengi wamepoteza makao na maafa kushuhudiwa, hivyo basi nimeamuru chakula kutoka kwenye maghala ya kitaifa kusambazwa kwa wahanga wa mafuriko,” akasema.
Isitoshe, kutokana na changamoto zinazoendelea kutokana na mvua nyingi, nafasi nyingi za ajira zimepotea, maeneo ya Tana River, Masinga na Ukanda wa Bahari ya Hindi yakiangaziwa.
Kwa upande mwingine, ametaka wizara inayoshughulikia mipango maalumu kushirikiana na washikadau kuhakikisha manusura wanafikiwa na misaada katika kila pembe ya nchi.
Hii ikiwa ni pamoja na serikali kuweka mipango ya kuwaondoa wanaokaa kwenye vyanzo vya maji.