Kimataifa

Vita vya Gaza: Mkuu wa Mashtaka ICC asaka kibali cha kumkamata Netanyahu

May 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA 

KIONGOZI wa Mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) Karim Khan ameiomba mahakama hiyo kutoa kibali cha kumkamata Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa makosa ya uhalifu wa kivita katika Ukanda wa Gaza.

Aidha, Bw Khan anataka kibali cha kumkamata kiongozi wa kundi la wapiganaji wa Hamas Yahya Sinmwar na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant.

Wengine anaopania kuwatia mbaroni ni wakuu wa Hamas- Mohammed Diab Ibrahim al-Masri na Ismail Haniyeh.

Haniyeh ni kiongozi wa kitengo cha kisiasa cha kundi hilo la Kipalestina linalotawala Gaza.

Ombi la Khan sasa linamweka Netanyahu katika kapu moja na Rais wa Urusi Vladimir Putin, ambaye ICC imetoa kibali akamatwe kuhusiana na hatua ya nchi hiyo kuvamia Ukraine Aprili 24, 2022.

Jopo la majaji wa ICC sasa watachunguza ombi la kiongozi huyo wa kitengo cha mashtaka katika mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa (UN) yenye makao yake jijini The Hague, Uholanzi.

Kulingana na Khan, mashtaka dhidi ya Netanyahu na Gullant yanajumuisha “kufanikisha utekelezaji wa mauaji, kusababisha njaa kama chombo cha kivita, ikiwemo kuzuia uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu na kuwalenga raia kimakusudi katika mapigano.

Netanyahu alipopata habari kwamba ICC inapania kutoa kibali cha kumkamata alisema kuwa “waranti yoyote aina hiyo itakuwa kitendo kibaya kuwahi kutokea katika historia ulimwenguni.”

Alisema Israel inayo asasi huru za kisheria ambazo “huchunguza kwa kina aina zozote za ukiukaji wa sheria.”

Khan amesema mashtaka dhidi ya Sinwar, Haniyeh na al-Masri yanajumuisha “uangamiza, mauaji, kuweka watu mateka, ubakaji na unyanyasaji wa kingono kizuizini.”

“Ulimwengu ulishtuka mnamo Oktoba 7, 2024 watu walipotolewa kutoka vyumba vyao vya kulala, kutoka nyumba zao na kutoka kibbutzim (vijiji) mbalimbali nchini Israel,” Khan akasema akitaja vitendo hivyo kama vya kinyama.