Polisi wa kike atiwa nguvuni kufuatia ufyatuaji risasi ulioishia kuua mvulana, 19
GEORGE MUNENE NA LABAAN SHABAAN
KIFO cha mwanaume mmoja katika soko la Kiandai Kaunti ya Kirinyaga kimemchongea polisi anayetuhumiwa kufyatua risasi.
Maafisa wa polisi walikuwa wanashika doria Jumamosi usiku risasi ilipofyatuliwa na kusababisha mauti ya Derrick Gachoki mwenye umri wa miaka 19.
Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi Kirinyaga, Andrew Naibei alisema afisa huyo alikamatwa baada ya kisa hicho kuripotiwa.
“Afisa huyo yuko kizuizini. Tunataka kubaini kwa nini marehemu alipigwa risasi,” Bw Naibei alisema.
Aliomba familia na wakazi kuwa na subira uchunguzi ukiendelea.
Baada ya tukio hilo, wakazi wenye hasira waliandamana na kuvamia kituo cha polisi cha Kianyaga wakililia haki.
Hali ya wasiwasi ilitanda huku wakazi wakiapa kupiga kambi kituoni hadi afisa aliyehusishwa na kifo hicho aadhibiwe kisheria.
Hata hivyo, baadaye walitawanyika baada ya maafisa wakuu wa usalama kuwaahidi haki itatendeka.
Familia ilipigwa na butwaa ilipopokea ripoti ya mauti ya mwana wao.
“Bado tunashtuka kufuatia kifo cha mwana wetu,” alisema Bi Sicily Wangu, shangazi wa marehemu.
Familia hiyo ilisema haikuamini kuwa Bw Gachoki alikuwa amefariki hadi walipoona mwili wake kwenye dimbwi la damu.
“Gachoki alikuwa mtu mwema na sijui ni kwa nini walimuua, nimekuwa nikiishi naye tangu 2008 mamake alipofariki,” akasema Bi Jane Muthoni, nyanyake marehemu.
Bw Gachoki alikuwa akicheza mchezo wa pool table na rafiki zake alipokumbana na kifo chake.
“Tulikuwa tukicheza mchezo huo na ghafla maafisa wa polisi walifika na tukaanza kutoroka. Muda mfupi baadaye tuliarifiwa Gachoki aliuawa kwa kupigwa risasi na mwili wake kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti,” akasema Bw Alex Njeru, rafiki wa marehemu.
Diwani wa wadi ya Baragwi David Mathenge alikashifu kisa hicho na kuwataka polisi kukamilisha upelelezi haraka iwezekanavyo.
“Tunataka kujua kama ni uhalifu kucheza mchezo wa pool table, tunalichukulia suala hili kwa uzito unaostahili,” alisema Bw Mathenge.