Habari Mseto

Serikali kutumia Sh300m kuhesabu wanafunzi

May 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MUMBI WAINAINA

SERIKALI imezindua mpango wa kuhesabu wanafunzi kote nchini utakaogharimu Sh300 milioni.

Katibu katika Wizara ya Elimu, Belio Kipsang, alisema Alhamisi kuwa, sensa hiyo itaendelezwa kwa kipindi cha siku 50.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa shughuli hiyo katika shule ya upili ya wasichana ya Moi, Nairobi, Dkt Kipsang alisema sensa hiyo itatekelezwa hadi shule zitakapofungwa.

Shughuli hiyo inaendeshwa na Shirika la Kitaifa la Takwmu (KNBS) kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu.

“Nafahamu tuna data kwenye mifumo yetu. KNBS hufanya tafiti na kutoa takwimu kila mwaka. Ni vizuri kuthibitisha baadhi ya data na takwimu ili tuweze kuzingatia hali halisi na yale ambayo mmekuwa mkipata,” akasema Dkt Kipsang.

Kwa mujibu wa KNBS, wanafunzi wengi walikuwa hawajaanza shule wakati sensa ya kwanza ya shule ilipofanyika mnamo 2007.

Lengo kuu la sensa ni kupata data na takwimu sahihi kuhusu shule na miundombinu yake.

Inatarajiwa kugharimu takriban 300 milioni. Kwa mujibu wa Dkt Kipsang, kufikia shule kufungwa sensa itakuwa imekamilika.

Katibu katika Wizara ya Elimu, Belio Kipsang. PICHA | MAKTABA

Dkt Kipsang aliendelea kusema kuwa, sensa inafanywa ili kuthibitisha idadi na kuhakikisha inalingana na matarajio ya nchi.

Takwimu zitaangaliwa, ambazo zinahusisha rejista ya shule, idadi ya walimu, miundombinu na vifaa vya kusomea. Baada ya kipindi cha siku 50, data itakuwa imechambuliwa na ripoti kuaandaliwa na kusambazwa kitaifa.

Dkt Kipsang alishughulikia suala la walimu ambao wako katika mazoezi ya ufundishaji na kusema, ikiwa watakuwa na uvumilivu kidogo, basi watakuwa wamefika wanapokwenda. “Walimu hawa wanahitaji kujua kwamba hii ni kama safari nyingine. Wanahitaji kuwa na uhakika wa hatima na kuzingatia hatima hiyo,” alisema.