Kimataifa

Zuma aapa kupigania haki zake baada ya kukaushiwa ubunge

May 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MASHIRIKA

JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

ALIYEKUWA Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameshikilia kuwa atapigania haki yake baada mahakama ya kikatiba nchini humu kumzima kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika wiki ijayo.

Katika uamuzi iliyoutoa Jumatatu wiki hii, mahakama hiyo yenye hadhi ya juu zaidi Afrika Kusini ilisema kuwa ilichukua hatua hiyo kwa misingi ya hukumu ya miezi 15 gerezani aliyopewa Zuma 2021.

Kulingana na Katiba ya nchi hiyo, mtu yeyote aliyehukumiwa kifungo cha angalau miezi 12 gerezani hafai kushikilia kiti cha ubunge.
Uamuzi wa mahakama ya kikatiba hauwezi kubatilishwa.

“Majaji wa mahakama ya kikatiba amefikia uamuzi kwamba siwezi kutekeleza uhuru wangu, demokrasia yangu,” Zuma akasema Alhamisi kwenye video katika mtandao wa YouTube iliyosambazwa na chama chake, uMkhonto we Sizwe (MK).

“Nitapigania haki zangu hadi nchi hii ikubali kwamba uhuru sharti uwe mkalifu, isiwe kwa baadhi ya watu huku wengine wakidhulumiwa.”

Ingawa jina la Zuma litaondolewa kutoka orodha ya wagombeaji ubunge wa chama cha MK, picha yake itasalia katika karatasi za kupigia kura kwa sababu yenye ndiye kiongozi aliyesajiliwa wa chama hicho.

Zuma aliunga mkono MK Desemba 2023 alipotangaza kuwa hangekifanyia kampeni chama tawala cha African National Congress (ANC) alichoongoza kuanzia 2007 hadi 2017.

Alijiuzulu kama rais wa Afrika Kusini mnamo 2018, kufuatia shinikizo kutoka kwa wandani wa kiongozi wa sasa Cyril Ramaphosa katika chama hicho.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma akizungumza na wanahabari nyumbani kwake kabla ya kuanza kifungo. PICHA | MAKTABA

Uongozi wake wa miaka tisa ulizongwa na tuhuma za ufisadi dhidi yake na kudumaa kwa ukuaji wa uchumi.

Kusukumwa gerezani kwa Zuma mnamo 2021 kulichochea fujo katika mkoa wa KwaZulu-Natal, anakotoka, hali iliyochangia kuuawa kwa zaidi ya watu 300.

Hata hivyo, hakutumikia kifungo hicho, kwa kosa la kudharau mahakama, kwani aliachiliwa huru kwa sababu kuugua ugonjwa usiojulikana.