Habari Mseto

Mshtuko wa walimu kuambiwa bima ya matibabu haijalipiwa na serikali

May 25th, 2024 1 min read

NA VITALIS KIMUTAI

WALIMU wanaotegemea bima ya afya ya Minet wamenyimwa huduma za matibabu baada ya Hazina ya Taifa kushindwa kutoa fedha ya kugharamia matibabu yao.

Ronald Mitei, mwalimu katika Shule ya Msingi ya Mogindo, Kaunti ya Bomet asema mwanawe wa umri wa miaka 10 hakupata matibabu katika Hospitali ya AGC Tenwek kwani alitakiwa alipe pesa taslimu.

“Kama mwalimu ambaye nimeajiriwa na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC), na ambaye nina bima ya Minet, nilitarajia mtoto wangu atibiwe bila shida,” Bw Mitei aliambia Taifa Leo.

Hata hivyo, alishtuka alipofahamishwa kuwa alipaswa kulipia huduma hiyo kwa fedha taslimu kwa sababu Minet haijatoa malipo ya matibabu ya mtoto wake kutokana na madai ya ‘masuala ya kifedha na kiufundi.’

“Nilijaribu kutumia kadi ya mke wangu, ambaye pia ni mwalimu, lakini matokeo yalikuwa yale yale – idhini ya awali ilikuwa haijaidhinishwa. Kisha tukachagua kutumia Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) na kuongeza Sh710 ili apewe dawa,” Bw Mitei alifichua.

Hazina ya Kitaifa imelaumiwa kwa kuchelewa kutoa Sh17.6 bilioni kwa TSC kwa mpango wa matibabu wa kila mwaka, na kuwaacha walimu na wakufunzi 406,635 bila huduma muhimu za afya.