Habari Mseto

Jinsi Kadhi Mkuu ameingilia kati vita vikali baina ya mke na mume

May 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA BRIAN OCHARO

KADHI Mkuu ametoa maagizo ya kuzuia mwanamume kumfukuza mkewe kutoka kwenye nyumba yao ya ndoa au kuchukua kitu chochote, hadi kesi kuhusu mgogoro wa mali kati ya wanandoa hao isikizwe na kuamuliwa.

Kadhi Mkuu Abdulhalim Athman alisema kuwa, mwanamke huyo aliyetambulika kama MAM, atapata madhara yasiyoweza kurekebishwa iwapo atafukuzwa kwenye nyumba ya ndoa na vitu vya nyumbani kuchukuliwa.

“MAM hana mahali pengine pa kwenda na haki yake ya nyumba na malazi itakiukwa,” alisema.

Rekodi za mahakamani zinaonyesha kuwa mume hufanya kazi ng’ambo.

Wakati uo huo, Kadhi Mkuu alitoa agizo la muda kwamba usimamizi wa mali hiyo uwe chini ya wakala huku mgogoro kati ya wanandoa hao kuhusu umiliki wake ukitatuliwa.

Maajenti hao watachaguliwa na mawakili wa wanandoa hao na kuidhinishwa na Mahakama Kuu kabla ya kuchukua usimamizi wa mali hiyo, ambayo inajumuisha nyumba za kukodisha na kukusanya kodi.

“Malipo ya kodi yatagawiwa asilimia 35 kwa mwanamke na asilimia 65 kwa mwanaume wakati suala la umiliki linasubiri kutatuliwa,” Kadhi Mkuu Athman alisema.

Hata hivyo, Kadhi Mkuu aliamua kwamba mwanamme huyo aliyetambuliwa kama COR, ametoa mchango mkubwa katika ujenzi na uendelezaji wa nyumba za kupangisha.

“Kwa hivyo atapata hasara zaidi kuliko MAM ikiwa maagizo anayotafuta Bi MAM yatakubaliwa kama alivyoyawasilisha,” alisema.

Kwa kuwa pande zote mbili zitapata hasara, Sheikh Athman aliagiza kodi ikusanywe na kugawanywa kwa kuzingatia michango ya kila mmoja wao hadi mgogoro huo utakapotatuliwa.

Mwaka jana, mwanamke huyo alienda kortini kuomba amri za muda dhidi ya mwanamume huyo, familia yake au wawakilishi wake kuwazuia kuingia, kujenga, au kuvuruga shughuli katika nyumba yao ya ndoa, mali, na haki zake za umiliki.

Alilalamika kwamba COR alitishia kuwafurusha wapangaji kutoka kwa nyumba za kukodisha na kukusanya vitu vyote vya nyumbani kutoka kwa nyumba ya ndoa.

Mwanamume huyo hata hivyo alipinga ombi hilo na kuomba litupiliwe mbali.

Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa wanandoa hao walifunga ndoa ya Kiislamu zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Awali, waliishi pamoja katika nyumba za kupangisha za mamake mwanamke huyo kabla ya kushirikiana kupata kiwanja kwenye shamba la mamake na kujenga nyumba za vyumba vitatu vya kulala.

Mwanamume huyo alifanya kazi nje ya nchi na mara kwa mara alimtembelea mkewe nchini Kenya.

Mnamo 2011, walinunua kiwanja cha ziada karibu na nyumba yao ya ndoa na kujenga nyumba za kukodisha.

Baada ya kukamilika kwa mradi huu, umiliki na usimamizi wake umekuwa suala la ugomvi kati ya wanandoa hao.

Mahakama ilibaini kuwa wahusika bado wako kwenye ndoa chini ya sheria za Kiislamu, kuwa mali yote ilipatikana wawili hao wakiwa kwenye ndoa na pia kuwa nyumba hizo zilijengwa kwenye ardhi iliyokuwa ikimilikiwa na jamaa za mwanamke huyo.