Habari Mseto

Ni njaa ya miezi mitatu kwa wafanyakazi 3,000 wa kaunti mishahara yao ikikawia

May 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na VITALIS KIMUTAI

WAFANYAKAZI 3,000 wa Serikali ya Kaunti ya Bomet wanaendelea kupitia kipindi kigumu kwa kuwa bado hawajalipwa mshahara wao kwa muda wa miezi mitatu iliyopita.

Gavana wa kaunti hiyo, Prof Hillary Barchok na Katibu wa Kaunti Simeon Langat wanadai hali hiyo imetokana na Hazina Kuu ya Kifedha kukosa kuwasilisha pesa kwa wakati unaohitajika.

“Tunafahamu kuwa mishahara ya Aprili kwa wafanyakazi wetu imechelewa. Hii imetokana na Hazina Kuu kuchelewa kuwasilisha fedha za Machi, Aprili na Mei,” ikasema barua iliyotiwa saini na Bw Langat.

“Lengo la waraka huu ni kuwarai wafanyakazi wetu wavumilie tunapopitia kipindi hiki kigumu. Tutalipa mishahara punde tu tukipata pesa hizo kutoka kwa Hazina Kuu ya Kifedha,” ikaongeza barua hiyo ya Mei 20.

Profesa Barchok alikiri kuwa serikali yake inakabiliwa na matatizo chungu nzima ya kifedha kutokana na kucheleweshwa kwa hela hizo.

Narai wafanyakazi na wanakandarasi wavumilie tu. Najua hawajalipwa,” akasema Barchok.