Habari Mseto

Mwanamke aliyedai ni daktari wa Raila Odinga afunguliwa kesi ya kulaghai Mnigeria

May 28th, 2024 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA aliyetumia jina la Raila Odinga kumtapeli mwekezaji kutoka Nigeria Sh25 milioni katika kashfa ya kuuzia mamlaka ya usambazaji wa dawa (KEMSA) neti zilizotibiwa ameshtakiwa kwa ulaghai.

Faith Mwikali Ndiwa anadaiwa alimwonyesha Jude Olabwayo Veracruz kandarasi ya kuuzia Kemsa neti zilizotibiwa za kuua mbu wanaosababisha gonjwa la malaria.

Kandarasi hizo zilikuwa zimepewa kampuni zake mbili Ashley Dylan Limited na Faizel Limited.

Kiongozi wa mashtaka Naomi Wanjiru alimweleza Shitubi kwamba Mwikali alimweleza Veracuz kampuni hizi zake Ashley Dylan na Faizel zilikuwa zimeshinda zabuni nambari IFT NO GF ATM MAL NFM-19/20-OIT-004 ya kuuzia Kemsa neti zilizotibiwa za kudumu muda mrefu-(LLINs).

Bi Wanjiru aliongeza kusema Veracruz alieleza polisi mshtakiwa alimweleza kandarasi hii ilikuwa imepewa mkwewe kinara wa Azimio Raila Odinga na kwamba amepungukiwa na fedha.

Mkwewe huyo Raila Odinga alikuwa anahitaji msaada ndipo Mwikali akamrai Veracruz atoboke pesa za kukamilisha zabuni hiyo kisha apate faida kubwa.

Veracruz alimpa Mwilkali Sh25 milioni ndipo hatimaye akagundua ametapeliwa.

Mwikali alikana mashtaka manane ya kumtapeli Veracruz kati ya Juni na Desemba 2022 Kaunti ya Nairobi.

Aliomba aachiliwe kwa dhamana lakini Bi Wanjiru akapinga akisema afisa wa polisi Bi Eunice Njue anayechunguza kesi hiyo “anahitaji muda kuwasilisha afidaviti inayosimulia sababu za kupinga mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.”

Hakimu mkuu Susan Shitubi aliamuru Mwikali azuiliwe katika gereza la Lang’ata hadi Mei 28,2024 atakaporudishwa kortini kuwasilisha upya ombi la kuachiliwa kwa dhamana.

Hakimu alielezwa Veracruz angelimpa Mwikali pesa zake kama angelionyeshwa zabuni hiyo na kuelezewa ilikuwa ya mkwewe Odinga.

“Afisa anayechunguza kesi anahitaji kupewa fursa ya kuandaa afidaviti akitoa sababu za kupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana,” hakimu mkuu Susan Shitubi alisema.