Habari Mseto

Tume yataka kaunti 10 zinazoitwa majina ya kikabila zibadilishwe

May 29th, 2024 1 min read

NA STEVE OTIENO

TUME ya Uwiano na Utangamano (NCIC) inataka kaunti 10 zibadilishwe majina.

Akizungumza jana jijini Nairobi, mwenyekiti wa tume hiyo, Askofu Samuel Kobia, alisema tayari kuna harakati za kuunda hoja ipelekwe bungeni kubadilisha majina ya kaunti hizo, anayosema ni ya kikabila.

“NCIC itapendekeza kuwasilishwa kwa hoja bungeni ili kaunti ambazo zinatambulika kwa majina ya makabila, zibadilishwe majina hayo. Tumejitolea kuhakikisha kuwa Wakenya wanaishi kwa amani, na kwamba walio wachache hawajihisi kama wasio na haki katika kaunti husika,” akasema.

Kaunti hizo10 ni Meru, Tharaka Nithi, Nandi, Kisii, Turkana, Embu, Samburu, Taita Taveta, West Pokot na Elgeyo Marakwet.

Bw Kobia alisema lengo hasa ni kuondoa ubaguzi dhidi ya makabila madogo katika kaunti zenye majina ya makabila makubwa. Mojawapo ya changamoto kuu za amani na utangamano katika ugatuzi ni mizozo ya mipaka.

NCIC inakisia kuwa kaunti 33 kati ya 47 nchini zinazozania mipaka.