Kimataifa

Kura zapigwa Afrika Kusini ushawishi wa ANC ukiyumba kwa mara ya kwanza katika miaka 30

May 30th, 2024 2 min read

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

RAIA wa Afrika Kusini walianza kupiga kura Jumatano katika uchaguzi mkuu ambao unaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini humo ikiwa chama tawala cha African National Congress (ANC) kitapoteza udhibiti wake bungeni.

Hii ni kulingana na matokeo ya hivi punde ya kura za maoni zinazoonyesha kupungua kwa ushawishi wa ANC.

Wapigakura watawachagua wawakilishi katika mabunge ya mikoa tisa na wawakilishi katika bunge la kitaifa, ambao watachagua rais mpya.

Ikiwa chama cha ANC kitazoa chini ya asilimia 50 ya kura za kitaifa, kitalazimika kusaka ushirikiano na vyama vingine ili kiweze kuendelea kuongoza nchi hiyo.

Hiyo itakuwa ni serikali ya kwanza ya muungano ndani ya miaka 30 tangu ANC iingie mamlakani mnamo 1994 pale Hayati Nelson Mandela alipokuwa kiongozi.

Utawala wa ubaguzi wa rangi uliangamizwa mwaka huo.

Shughuli za upigaji kura zilianza saa kumi na moja alfajiri (au saa kumi na mbili asubuhi saa za Afrika Mashariki) na kufungwa saa kumi na moja jioni (au saa kumi na mbili saa za Afrika Mashariki).

Jumla ya wapigakura milioni 27 waliosajiliwa walitarajiwa kushiriki shughuli hiyo ya kidemokrasia.

Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini ilitarajiwa kuanza kutangaza matokeo ya muda ya uchaguzi saa chache baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria, tume hiyo inao muda wa hadi siku saba kutangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo.

Jana, raia Afrika Kusini waliendelea kuelezea wasiwasi wao kwamba huenda nchi hiyo ikawa chini ya utawala wa muungano wa vyama.

“Tuna wasiwasi kwani hatujui nini kitatendeka. Je, tutaongozwa na serikali ya muungano?” akauliza Amena Luke, 19, mwanafunzi, akiwa foleni kusubiri kupiga kura katika kituo cha Berario Recreation Centre, jijini Johannesburg.

Hata hivyo, duru zinasema kuwa chama cha ANC bado kitapata idadi kubwa ya kura kitaifa.

Hii ina maana kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba kiongozi wake Rais Cyril Ramaphosa atahifadhi wadhifa huo. Kiongozi huyo anaweza tu kupoteza kiti hicho ikiwa kutaibuka mpinzani ndani ya chama hicho ikiwa kitapata matokeo mabaya kinyume na ilivyotarajiwa.

Wapigakura wengi wameonyesha kukerwa na ongezeko la ukosefu wa ajira, visa vya uhalifu, visa vya kila mara vya kupotea kwa umeme na tuhuma za ufisadi zilizoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wa ANC.

Changamoto hizo zimechangia kushuka kwa umaarufu wa chama hicho tawala kwa kiwango kikubwa zaidi.

Foleni ndefu ilishuhudiwa nje ya kituo cha kupigia kura cha Shule ya Upili ya Midrand, katika mtaa wa kaskazini mwa Johannesburg, wapigakura wakisubiri zamu yao kuwachagua viongozi wapya.

Wengi walionekana kuvali mavazi mazito na kofia kujikinga na baridi ya majira ya asubuhi.

“Nimepigia kura chama cha EFF kwa sababu ninataka watu wenye mawazo mapya bungeni,” akasema Andrew Mathabatha, 40, mhandisi aliyewasili mapema katika kituo hicho kupiga kura. Alikuwa akirejelea chama cha Economic Freedom Fighters, kilichoasisiwa na mwanasiasa mbishani Julius Malema.