Zaidi ya Sh1 bilioni zilimezwa na miradi hewa Kaunti za North Rift – Ripoti
KAUNTI tisa katika Ukanda wa Bonde la Ufa zilipoteza karibu Sh1 bilioni kupita malipo ya kazi ambayo haikufanyika pamoja na matumizi mengine haramu.
Ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, ya 2022/23, imefichua kuwa kaunti hizo hazikutoa stakabadhi za kuthibitisha matumizi ya pesa ambazo zilitoka kwa serikali.
Bila stakabadhi hizo, kila kaunti inakisiwa ilipoteza mamilioni ya pesa.
Kaunti ya Kericho ililipa Sh29 milioni kwa wanakandarasi 15 ilhali hakuna ushahidi au ithibati ya kuonyesha kuwa bidhaa ziliwasilishwa au huduma zilitolewa kwa kaunti.
Pia kaunti hiyo ilitumia Sh169 kwenye safari za ndani ya nchi pamoja na marupurupu kwa maafisa 47. Hata hivyo, stakabadhi za benki zinaonyesha maafisa hao walilipwa pesa zaidi hata kuliko siku za mwaka.
Mbali na hayo, kaunti hiyo iliwalipa walinzi kutoka kampuni ya kibinafsi Sh2.4 milioni kwa kazi ambazo zingetekelezwa na maafisa wa ulinzi wa kaunti almaarufu kanjo.
Kaunti ya Turkana nayo iliwalipa wanakandarasi Sh18 milioni kwa ujenzi wa majengo japo hakukuwa na stakabadhi za kuonyesha malipo hayo.
Gavana wa Pokot Magharibi, Simon Kachapin, naye alilipa Sh5.8 milioni kwa viti 3,934 vya watoto katika shule za chekechea huku kila kiti kikinunuliwa kwa Sh1,499.
Hata hivyo, uchunguzi wa kitengo cha utoaji zabuni ulibaini kuwa kila kiti kilistahili kununuliwa kwa Sh900 na Sh599 zaidi zililipwa bila sababu zozote. Hii inaamanisha kuwa Sh2.3 milioni ziliishia kupotea kwenye kandarasi hiyo.
Pesa pia zilipotea katika Kaunti ya Samburu baada ya Gavana Lati Leleit kuwalipa vibarua wanaofanya kazi katika sekta ya afya Sh36,441. Kinaya ni kuwa vibarua hao walipewa ajira bila idhini ya Bodi ya Uajiri wala hawakupewa barua inayotoa mwelekeo kuhusu majukumu yao.
Pia kaunti hiyo huenda ilipoteza Sh5 milioni katika ununuzi wa mafuta na Sh7 milioni kwa kampuni ambayo huyakarabati magari ya kaunti.
Katika Kaunti ya Trans Nzoia, Gavana George Natembeya alimulikwa kwa kuwalipa vibarua 515 jumla ya Sh95 milioni kwa muda wa miezi miwili. Hii ni licha ya Serikali ya Kaunti kuwaajiri vibarua 682 kwa zaidi ya miezi mitatu ambayo imewekwa kwenye sheria.
Ubadhirifu pia ulishuhudiwa Uasin Gishu ambapo Gavana Jonathan Bii, bila kufuata sheria, aliajiri mshauri wa masuala ya kisheria ambaye alimlipa Sh6 milioni. Hata hivyo, hakukuwa na ushahidi kuwa huduma hizo za uwakili zilishindaniwa kabla ya ajira kutolewa.
Kaunti ya Baringo ilitumia Sh200 milioni kuyanunua mafuta lakini hakuna stakabadhi zozote za kuthibitisha matumizi hayo.
Vilevile, ilitumia Sh151 milioni kununua mafuta ya magari na vifaa vilivyotumika katika ujenzi wa barabara lakini pia stakabadhi za kuthibitisha matumizi hayo hazipo.
Katika Kaunti ya Narok, kima cha Sh59 milioni ilitumiwa kuyanunua magari na vifaa vya uchukuzi. Hata hivyo, ilibainika kuwa magari hayo hayakununuliwa na kaunti kwa kuwa iliyakodisha tu.