Habari Mseto

IPOA yachunguza madai mtoto mchanga aliyefia kituoni alizabwa kofi na polisi

June 6th, 2024 1 min read

NA JAEL MAUNDA

MAMLAKA Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) imeanzisha uchunguzi kuhusiana na kifo cha mtoto wa umri wa mwaka mmoja na nusu aliyefariki baada ya kudaiwa kuzabwa kofi na afisa wa polisi.

Kisa hicho kinadaiwa kufanyika katika kituo cha polisi cha Kambu, Kaunti ya Makueni.

Bi Zipporah Mutheu na mwanawe walikamatwa na maafisa wa polisi mnamo Mei 29 na kupelekwa katika kituo cha polisi.

Mwenyekiti wa IPOA, Bi Anne Makori alisema maafisa wa mamlaka hiyo walitembelea eneo la tukio na kufanya mahojiano na mashahidi na baada ya kukamilisha uchunguzi, watapendekeza watakaothibitishwa kuhusika washtakiwe.

“Mnamo Ijumaa, Mei 31 IPOA ilianzisha uchunguzi kwa hiari yake kuhusu kifo cha mtoto mdogo katika kituo cha polisi cha Kambu kilichoko Makueni, ambako mama yake, Zipporah Mutheu, alikuwa amezuiliwa. Maafisa wa IPOA pia wametembelea eneo hilo na hadi sasa wamehoji mashahidi kadhaa. Baada ya kukamilisha uchunguzi na pale ambapo itathibitishwa makosa ya jinai yalifanywa, IPOA itapendekeza wahusika washtakiwe,” alisema Bi Makori kwenye taarifa.

Kisa hicho kilifanyika wakati polisi walimkamata Zipporah Mutheu kwa kutolipa deni la mtu. Polisi waliingilia kati kutatua mzozo huo.