Watetezi wa muguka wataka Wizara ya Usalama kulinda mmea huo
Na GEORGE MUNENE
WADAU kutoka kaunti za Embu, Kirinyaga, Meru na Tharaka Nithi wanaendelea kuishinikiza Wizara ya Usalama wa Ndani ilinde biashara ya muguka inayopingwa katika kaunti za Pwani na Kaskazini Mashariki.
Wakulima na wafanyabiashara wa zao wanaitaka wizara hiyo kuchukua hatua kuhakikisha agizo lililotolewa na mahakama Mei 28 kwamba biashara hiyo isiwekewe vikwazo bali iheshimiwe.
Wengine wanaotaka biashara hiyo ilindwe ni wabunge na maseneta, madiwani na Gavana wa Meru Cecily Mbarire.
Aidha, wameitaka Wizara ya Usalama inayoongozwa na Waziri Kithure Kindiki kuamuru kuachiliwa huru kwa wafanyabiashara wa muguka ambao walikamatwa kutokana na sababu zisizojulikana sehemu mbalimbali nchini wakiendelea na biashara zao.
Aidha, wameitaka Wizara ya Kilimo kuhakikisha utekelezaji mkamilifu wa Sheria ya Mazao ya 2023 na Kanuni kuhusu Miraa na Muguka.
Gavana Mbarire alisema marufuku iliyowekwa na serikali za kaunti za Pwani kuhusu biashara ya muguka ni haramu.
“Aidha, hatua ya serikali za kaunti za Pwani ya kuongeza ada zinazotozwa wafanyabiashara wa muguka si halali na hatua hiyo inapasa kubatilishwa. Muguka haifai kuchukuliwa kama zao tofauti na mazao mengine ambayo yameidhinishwa na serikali,” Bi Mbarire akasema.
Viongozi hao walilalamika kuwa kuwekwa kwa viwango tofauti vya ushuru na ada nyinginezo zinazotozwa muguka ikilinganishwa na mazao mengine kunaweza kutoa nafasi kwa kaunti zingine kuunda sheria zao zinazokiuka Katiba ya Kenya sheria nyinginezo za nchi.
Wadau hao walimtaka Rais William Ruto kuingilia kati na kutatua mzozo kuhusu muguka.
Hii ni baada ya magavana na viongozi kutoka Pwani kufeli kufika katika mkutano wa wadau uliofanyika mjini Machakos.
“Tunathamini kujitolea kwa Rais katika kulishughulikia suala hili, tunahisi kwamba anapaswa kuitisha mkutano utakaoshirikisha wadau wote wakiwemo magavana wa kaunti za Pwani waliodinda kuhudhuria mkutano wa Machakos. Tunataka mwelekeo na suluhu la mwisho kwa mzozo huo,” akakariri Gavana Mbarire.
Viongozi hao walisisitiza kuwa muguka ni zao halali kama vile kahawa, majani chao na mnazi na hamna anayepaswa kuzuia kuuzwa kwake nchini.
Walidai kuwa, kisayansi, muguka haina madhara yoyote kwa mwili wa mwanadamu na hivyo wafanyabiashara wa zao hawafai kuingiliwa kwa njia zozote zile.
Walisema kuwa muguka huzalisha mapato ya kima cha Sh13.1 bilioni kwa taifa hili kando na kutegemewa na zaidi ya watu 1.4 milioni.
“Watu wengine wengi wanafaidi kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na sekta hii ndogo ya muguka,” akaongeza Bi Mbarire.