Ununuzi wa nyumba ya kifahari wakwama baada ya kifo cha mwekezaji
NA SIAGO CECE
UUZAJI wa nyumba yenye thamani ya Sh30 milioni umekwama baada ya kifo cha mwekezaji wa Kiswisi, Heinz Rubi, aliyekuwa akitaka kununua nyumba hiyo huko Diani, Kaunti ya Kwale.
Bw Rubi alikuwa ameanza mchakato wa kununua ardhi yenye ekari nukta 0.1 na nyumba ya kisasa kutoka kwa mfanyabiashara Stella Kilonzo mapema mwaka 2024 alipougua na kuaga dunia Aprili 2, 2024, katika hospitali moja jijini Mombasa.
Hali hii imeleta mvutano kati ya Bi Kilonzo na wakili wake baada ya kugundua kuwa raia huyo wa kigeni alikuwa ameweka Sh24 milioni kwenye akaunti ya wakili huyo zikisubiri kukamilishwa kwa uuzaji kisheria.
Kulingana na makubaliano yao tarehe Januari 9, 2024, Bi Kilonzo alipokea Sh6 milioni kama malipo ya awali ya asilimia 20. Kiasi kilichobaki cha Sh24 milioni kilitakiwa kupelekwa kwa wakili wake baada ya kukamilika kwa uhamisho.
Mkataba huo ulipigwa saini na Bi Kilonzo, wakili wake Sheila Muthee wa Muthee and Partners LLP na marehemu Bw Rubi.
Mchakato mzima ulikuwa uchukue siku 45 kutoka tarehe ya malipo ya amana ambayo ilifanyika Januari 11.
Bi Kilonzo sasa anadai wakili wake, Sheila Muthee, ameshindwa kutoa fedha hizo licha ya kupokea malipo yote.
Amewasilisha malalamiko kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Malalamiko ya Mawakili (ACC).
“Niliagiza afanye mchakato wa kisheria na kuuza nyumba yangu huko Diani. Alitakiwa kunilipa asilimia 80 iliyobaki lakini hapokei simu zangu wala kujibu baruapepe zangu na zile za wakili wa mteja wangu,” alisema Bi Kilonzo katika malalamiko yake kwa afisi za ACC.