Habari Mseto

Aliyechafua madhabahu kwa kwenda haja kwenye sanamu ya Yesu asakwa na polisi

June 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA KASSIM ADINASI

POLISI katika eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya wanamsaka mwanaume mmoja aliyenaswa kwenye kanda za CCTV akienda haja kubwa kwenye sanamu ya Yesu Kristo iliyokuwa kwenye madhabahu ya Kanisa Katoliki la St Andrews’ Bondo.

Padre Edwin Obudho wa Parokia hiyo alitoa ripoti hiyo katika kituo cha Polisi cha Bondo na kutaja kitendo hicho kuwa kibaya na cha ajabu.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Siaya, Cleti Kimaiyo, Padre Obudho alidai kwamba mnamo Jumanne Juni, 4, 2024, viongozi wa kanisa hilo waligundua kuwa sanamu ya Yesu Kristo iliyokuwa kwenye madhabahu ya kanisa karibu na Ekaristi Takatifu haikuwepo.

Hii iliwafanya viongozi wa kanisa hilo kukagua picha za CCTV.

“Hapo ndipo walipogundua kwamba mwanaume mmoja alikuwa ameingia kwenye kanisa hilo akiwa amevalia shati la mistari nyeusi na nyeupe na suruali nyeusi,” akaeleza bosi huyo wa polisi.

Mwanamume huyo, ambaye bado hajatambuliwa, aliingia kanisani jioni wakati waumini wengine walipokuwa wakifanya maombi yao ya kawaida.

“Baada ya uhakiki wao wa picha za CCTV tarehe 6/6/2024, iligunduliwa kuwa mwanaume huyo aliingia ndani ya ukumbi wa kanisa jioni hiyo wakati waumini walikuwa wakiomba,”

“Kisha mshukiwa huyo alisubiri hadi waumini wengine wa kanisa hilo walipoondoka na baadaye kuenda hadi eneo ambalo sanamu ya Yesu ilitundikwa na kuiondoa,”

“Aliibeba hadi kwenye jumba la juu ambapo aliiweka sakafuni, akashusha suruali yake na kuenda haja kubwa. Alipomaliza, alifunika kinyesi chake kwa kutumia karatasi na kuificha sanamu hiyo chini ya kiti na kuondoka,” ripoti hiyo ilisema zaidi.

Bw Kimaiyo alisema kuwa maafisa wa upelelezi wanaendelea kufuatilia suala hilo na watakuwa wakishirikiana na waumini wa kanisa hilo ili kumtambua mshukiwa huyo na pia kubaini kiini cha kitendo hicho cha ajabu.