Dereva anusurika gari la mbunge likiteketea ajalini usiku
DEREVA wa Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya (pichani) anauguza majeraha baada ya gari la mbunge huyo kuhusika katika ajali mbaya Jumapili usiku.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Roka kwenye barabara kuu ya Kilifi-Malindi wakati Bw Omar Keah, dereva, alipokuwa akielekea kumchukua mbunge huyo katika Uwanja wa Ndege wa Malindi.
Gari hilo aina ya Mercedes Benz liliteketea kwa moto baada ya kugonga lori lililokuwa likielekea upande sawia mwendo wa saa moja unusu usiku, kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kilifi Kaskazini, Bw Kenneth Maina.
“Tulifahamishwa kuhusu ajali iliyotokea jana jioni iliyohusisha gari la Mercedes Benz, nambari ya usajili KDJ 550M ambalo ni la Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya. Dereva wake ndiye aliyehusika katika ajali hiyo ambapo aligonga lori lenye nambari ya usajili KBS 199L na gari likashindwa kudhibiti na kuwaka moto,” akasema.
Bw Maina alisema dereva huyo aliokolewa na umma na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kilifi.
“Dereva alivunjika mkono na kwa sasa yuko katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) ila hayuko kwa hatari,” aliongeza.
Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa alisema alimpigia simu dereva wake saa kumi na mbili jioni alipokuwa Nairobi ili kumchukua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Malindi.
Alithibitisha kuwa dereva alikuwa anaenda kumchukua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Malindi wakati wa tukio.
“Mwendo wa saa kumi na mbili jioni nilimpigia simu dereva wangu nilipokuwa nikiabiri ndege Nairobi na nilipofika Uwanja wa Ndege wa Malindi nilipigiwa simu na kujulishwa kuwa gari lilikuwa limepata ajali na dereva wangu alijeruhiwa,” alisema.
Bw Baya alisema kuwa gari hilo liliteketea kabisa lakini akamshukuru Mungu kuwa dereva wake angali hai.
“Nipo salama na tunamshukuru Mungu kwa kuwa dereva wangu yu hai na tunamuombea kwa Mungu apate nafuu ya haraka,” alisema.
Walioshuhudia walisema kuwa, Bw Keah aliokolewa na wanawake wawili waliokuwa wakitoka Malindi kuelekea Kilifi.
Wanawake hao walifika punde baada ya ajali na kumvuta dereva kwenye paa wazi la gari.
Mara baada ya hapo, gari hilo liliteketea kwa moto na wakamkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kilifi kwa gari lao.
Bw Maina alisema magari yote mawili yatavutwa hadi kituo cha polisi.