Kimataifa

Israel yaua 274 kambini Gaza ikiokoa mateka 4 raia wake

June 10th, 2024 2 min read

GAZA, PALESTINA

WANAJESHI wa Israeli mnamo Jumamosi waliwaua watu 274 wakiwemo watoto katika kambi ya wakimbizi Ukanda wa Gaza.

Taarifa kutoka kwa Wizara ya Afya ya utawala wa kundi la Hamas, jana ilisema wanajeshi wa Israeli walivamia kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, Gaza ya kati na kuwaua watu hao hao, yakiwa mauaji mabaya zaidi kuwahi kutekelezwa.

Hamas, kadhalika ilisema kuwa zaidi ya watu 698 walijeruhiwa, wengine vibaya mno.

Israeli ilitekeleza shambulizi hilo kuwanasua raia wake ambao walikuwa wameshikwa mateka na kundi la Hamas.

Raia wa Israeli walionusuriwa ni Noa Argamani, 26, Almog Meir Jan, 22, Andrei Kozlov, 27, na Shlomi Ziv, 41. Waliokolewa baada ya kushikwa mateka na Hamas mnamo Oktoba 7, 2023 wakati wa tamasha moja ya muziki Kusini mwa Israeli.

Kwa upande mwingine, wanajeshi wa Israeli walikadiria idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi ya Jumamosi kuwa watu 100.

Wakimbizi wanaoishi katika kambi hiyo ya Nuseirat walisema kuwa mashambulizi hayo ya Israeli yalikuwa mabaya na yalitekelezwa na wanajeshi kupitia ndege ya angani.

“Baadaye miili ya watu ilitapakaa kote na damu kumwagika kila mahali,” akasema shahidi mmoja kwa jina Abdel Salam Darwish.

Wakati ambapo Hamas walikuwa wakiomboleza mauji hayo, kuokolewa kwa raia hao wanne kuliibua sherehe ya aina yake nchini Israeli na Amerika ambapo Rais Joe Biden alipongeza uokoaji huo.

Hata hivyo, Afisa wa Masuala ya Nje wa Muungano wa Mataifa ya Ulaya (EU) Joseph Borrell ilikashifu mashambulizi hayo na kusema hayakustahili.

“Kuna ripoti ya mauaji ya halaiki ya raia na haya yanasikitisha sana,” akasema Borell.

Picha kutoka kambi ya wakimbizi ya Nuseirat zilionyesha uharibifu mkubwa ambao ulikuwa umetekelezwa huku raia wakiwaomboleza wapendwa wao.

Usimamizi wa Hospitali za al-Aqsa na al-Awda ulisema ulikuwa umehesabu miili 70.

Hamas nayo ilisema watu 86 kati ya 274 waliouawa wakati wa oparesheni iliyochukua muda wa saa mbili, walikuwa raia wa Palestina.

Marwan Abu Nasser, daktari katika hospitali ya al-Aqsa alikiri kuwa hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kuwa hawana mochari za kuhifadhi miili ambayo ililetwa.

Awali Daniel Hagari ambaye ni afisa wa mawasiliano wa jeshi la Israel alisema idadi ya waliouawa ilikuwa chini ya watu 100. Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant naye alifichua kuwa mwanajeshi wao mmoja aliuawa na akaaga hospitalini baadaye.

Kuokolewa kwa mateka hao kumejiri wakati ambapo kumekuwa na wito wa kuzirai Israel na Hamas zisitishe vita ili zielewane.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amekuwa akikabiliwa na shinikizo za kuafikiana na Hamas ila mrengo wa kisiasa Israel unasisitiza kuwa vita pekee ndiyo njia ya kuwaokoa mateka wao Gaza.

Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh ambaye alikashifu mauaji hayo, alisema kuwa watalipiza kisasi.

Oktoba 7, Hamas ilitekeleza mashambulizi ambayo iliwaua watu 1,200 Kusini mwa Israel na wakawashika mateka watu 251.