Habari Mseto

Ndovu pia wanajuana kwa majina kama binadamu, utafiti mpya wabaini

June 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ONDIEKI

UTAFITI mpya umeonyesha kuwa ndovu wana sifa ya kipekee ambapo wao pia wanafahamiana kwa majina kama tu binadamu.

Utafiti huo ambao ulichapishwa kwenye Jarida la Kisayansi la Mazingira nchini Amerika, unasema kuwa ndovu huitana kwa majina na huelewana.

Utafiti huo ulifanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Colorado ambao waliwaita ndovu hao kwa majina yao nao wakaitikia kisha kufuata amri.

Wakishirikiana na Shirika la Kuwaokoa Ndovu dhidi ya uwindaji haramu, watafiti kutoka chuo hicho walitumia mashine kuthibitisha kuwa ndovu walikuwa wakiitana kwa majina yao na walijuana vizuri.

Walipotumia mashine hiyo kucheza sauti ambazo walikuwa wamezinasa, ndovu waliitikia na kufika kwao.

Mtafiti Michael Pardo aliwaongoza wenzake kufanya utafiti huo katika Chuo cha Colorado, Shirika la Kuwaokoa Ndovu wakishirikiana na mbunga moja nchini Kenya.

“Utafiti wetu unaonyesha kuwa ndovu hawategemei kuiga bali wanafuata sauti na kuzungumziana. Hii ni sawa na jinsi ambavyo binadamu hufanya,” ikasema utafiti huo.

Wanasayansi wanasema kuwa uwezo wa kijifunza na kutoa sauti mpya haupo sana katika wanyama lakini ni muhimu katika utambulishi miongoni mwao.