Hofu ya kuzagaa kwa mitandao ya filamu chafu za ngono zinazohusisha watoto
MAENEO karibu 200 jijini Mombasa yanafuatiliwa kwa karibu na polisi wanaoendeleza uchunguzi dhidi ya watu wanaoaminika kuwatumia watoto kutengeneza filamu za ngono zinazosambazwa mitandaoni.
Maafisa wa usalama wanaohusika katika uchunguzi huo waliambia Taifa Leo kwamba wamegundua kuwepo kwa walanguzi wa watoto katika jiji hilo ambao wanatumia watoto wadogo kupeperusha filamu chafu kwa watazamaji wa humu nchini na kimataifa.
Uchunguzi huu unafanywa wakati ambapo mitandao kadhaa ya kijamii pia iko lawamani kimataifa kwa kuruhusu uchapishaji wa video chafu.
Ijapokuwa maeneo mahususi yanayolengwa na maafisa wa ujasusi jijini Mombasa hayawezi kufichuliwa kutokana na hatari ya kuhatarisha uchunguzi, visa vya washukiwa wa ulanguzi wa binadamu na dhuluma za watoto vimewahi kuripotiwa awali katika maeneo ya Bamburi, Nyali na Mtwapa iliyo katika kaunti jirani ya Kilifi.
“Uchunguzi unaonyesha kuwa watoto wadogo wanaingizwa kwenye mtandao na kulipwa kima kisichopungua Sh6,000 kwa wiki. Waajiri wanatumia sarafu fiche za mitandaoni zinazopatikana wakati watoto wanapohusishwa katika video hizo chafu, kisha wanazibadilisha kuwa sarafu rasmi za pesa,” afisa wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) anayehusika katika uchunguzi wa visa hivyo alisema.
Mpelelezi huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa kukosa mamlaka ya kutoa maoni kuhusu suala hilo kwa wanahabari, alieleza kuwa ili kupata sarafu hizo za mitandaoni, ukurasa wa tovuti hufunguliwa kwanza kwa jina la mtu binafsi, ambayo ndiyo hutumika kupeperusha video za ponografia kwa wateja waliosajiliwa kwenye tovuti mahususi.
Wakazi katika baadhi ya maeneo walisema matukio ya aina hiyo yamekuwa yakiongezeka hasa yakilenga watoto kutoka katika familia zisizojiweza kimaisha.
Kulingana na mhubiri Patrick Muchiri wa Kanisa la The Bible Way Ministries lililoko Mtwapa, vijana wanaotafuta ajira pia wamekuwa wakiangukia mtego baada ya kudanganywa kuwa kuna nafasi za kazi lakini wanaishia kudhulumiwa kingono.
“Hili ni suala ambalo tumekuwa tukipokea ripoti nyingi kama wachungaji na pia ndani ya jamii zetu alisema.”
“Wapo watu wanaowaendea wenye changamoto za kiuchumi na kuwaambia wapo tayari kuwalea watoto wao ikiwa ni pamoja na kushugulikia elimu yao lakini mtoto akifika mjini mambo yanabadilika. Badala ya kupata elimu ambayo iliahidiwa, watu hawa wanaanza kumnyanyasa mtoto,” akaongezea.
Washukiwa
Mnamo Jumanne, wanawake wawili walishtakiwa kwa ulanguzi wa binadamu na kuendeleza ulanguzi wa watu baada ya watoto wawili kudaiwa kupatikana katika nyumba inayohusishwa na washukiwa hao jijini Mombasa.
Caren Atieno Okello na Flora Naomi Osendi walifikishwa mbele ya mahakama ya watoto ya Tononoka na kushtakiwa kwa makosa kadha ya ulanguzi wa watu, kula njama ya kutenda uhalifu na usambazaji wa machapisho machafu.
Huku Bi Okello akikiri mashtaka yote waliyosomewa isipokuwa mawili yanayohusu usafirishaji wa watoto hao, Bi Osendi alikana makosa yote zaidi ya saba.
Mahakama ilisikia kwamba wawili hao walifikiria kusafirisha mtoto wa miaka 17.
Washukiwa hao walinaswa mnamo Juni 10 na maafisa wa Kitengo cha Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu na Ulinzi wa Mtoto, wakiongozwa na Millicent Ouko.
Wakili wa upande wa mashtaka, Biasha Khalifa, aliiomba mahakama kuwanyima dhamana washukiwa hao akihofia kuwa huenda wakaingilia mashahidi kwa kuwatisha.
“Washukiwa hawana makazi maalum kwa hivyo itakuwa vigumu kuwatafuta ikiwa watapewa dhamana kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hii,” mwendesha mashtaka alisema.
Washukiwa hao wamedaiwa kuwa kwenye mtandao mkubwa na wakiachiliwa wanaweza kupanga njama ya kuwatisha mashahidi.
“Washtakiwa wote wawili waliishi katika makao ya kukodisha, kwa hivyo ikiwa wataachiliwa, inaweza kuwa vigumu kuwapata, na hivyo kuna hatari yao kutoroka,” mwendesha mashtaka alisema.
Wawili hao walizuiliwa rumande Shimo La Tewa hadi Julai 2, wakati hali halisi ya kesi hiyo itakaposomwa kwa Bi Okello kwa makosa ambayo amekiri hatia, na uamuzi wa masharti ya bondi pia yaelezwe kwa mshukiwa wa pili.