Wengine saba wauawa katika maandamano DRC
NA MASHIRIKA
BUTEMBO, DRC CONGO
WATU wasiopungua saba wameuawa katika jimbo la Kivu, eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, linalokumbwa na michafuko.
Haya yalijiri baada ya watu kuandamana barabarani wakilalamikia kuongezeka kwa mashambulizi ya kikatili yanayoshukiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Kiislamu (IS).
Kundi la Waasi kwa jina Allied Democratic Forces (ADF), linalohusishwa na IS, linadaiwa kuwaua watu zaidi ya 40 kwenye shambulizi lililotekelezwa katika kijiji cha Mayikengo wiki iliyopita na wengine zaidi ya 80 katika mashambulizi yaliyofanyika katika jimbo hilo wiki iliyotangulia.
“Hali ya ukosefu wa usalama umechochea hasira miongoni mwa raia na kusababisha mauaji ya wanajeshi wawili na dereva wao katika eneo la Lubero yaliyotekelezwa na umati ulioteketekeza gari lao Ijumaa usiku,” afisa wa eneo Julio Mabanga alieleza vyombo vya habari.
Bw Mabanga alisema kuwa Jumamosi, michafuko mingine yaliyozuka kati ya maafisa wa usalama na wakazi wa eneo hilo na kusababisha vifo vya watu wengine watatu, raia, mwanajeshi na ajenti wa Huduma ya Ujasusi Nchini humo (ANR).
Ghasia zingine zilizuka katika mji wa Butembo Jumamosi ambapo mamia ya vijana walifurika barabarani wakiwa wamebeba vijiti na kuimba nyimbo za kukemea kukithiri kwa hali ya ukosefu wa usalama.
Meya wa Butembo, Mowa Baeki Telly, alithibitisha kuwa raia mmoja aliuawa katika ghasia baina ya maafisa wa usalama na waandamanaji mjini humo.
Chimbuko la ADF ni taifa jirani la Uganda, lakini sasa imekita kambi katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa Congo.
Limetangaza kuunga mkono IS na limekuwa likitekeleza mashambulizi ya kila mara na kusababisha michafuko katika eneo hilo kwani makundi kadhaa ya waasi hushindania umaarufu na raslimali.