Mwanamume apoteza maisha kwenye ugomvi kuhusu unga
POLISI katika Kaunti ya Narok wanamzuilia mwanamume mwenye umri wa miaka 33 ambaye alidaiwa kumuua jirani yake wikendi iliyopita.
Imesemekana alitekeleza mauaji hayo baada ya wawili hao kugombana kuhusu unga wa pakiti mbili eneo la Olulunga.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Narok, Riko Ngare, Bw Nelson Lagat alidungwa kisu mara kadhaa na rafikiye ambaye ni jirani yake.
Bw Langat alikimbizwa hadi hospitali ya Kaunti ndogo ya Olulunga akitokwa na damu nyingi kwenye shingo, kifua na pia mgongoni.
Aliaga katika hospitali ya Longisa ambapo alifariki baada ya kufikishwa hospitalini humo.
Mshukiwa alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Olululunga ambako anaendelea kuzuiliwa akisubiri kufikishwa kortini mnamo Jumanne.
“Chifu alifahamishwa kuhusu tukio hilo na baadaye ikabainika kuwa marehemu alikimbizwa hospitalini na umma baada ya wawili hao kushuhudiwa wakipigana,” akasema Bw Ngare, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Narok.
Jirani mmoja alieleza Taifa Djitali kuwa, vita hivyo vilianza kama mzozo wa kawaida kabla ya kuishia kuwa mauti.
“Nilikuwa kwa nyumba na nikasikia sauti lakini nikafikiria ilitoka kwa wakulima ambao walikuwa wakivuna mimea yao. Kelele hizi zilipotanda zaidi, nilienda kufuatilia kile ambacho kilikuwa kimetokea,” akasema jirani huyo Mercy Korir.
“Hapo ndipo nilimpata mshukiwa akiwa amelala, akiwa ameloa damu huku akiguguna kwa uchungu,” Bi Korir akaongeza.
Mshukiwa anatarajiwa kushtakiwa kwa mauaji mnamo Jumanne, Juni 18, 2024.