Habari

VITIMBI: Wavulana waitwa shule za wasichana

January 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

Baadhi ya wanafunzi waliofanya mtihani wa Darasa la Nane 2018 hawataweza kujiunga na Kidato cha Kwanza kuanzia Jumatatu, baada ya kuitwa shule za jinsia tofauti.

Hayo yaliibuka Ijumaa huku Wizara ya Elimu ikilaumiwa kwa sera yake mpya inayonyima walimu wakuu uwezo wa kusajili wanafunzi shuleni moja kwa moja. Siku moja kabla ya wanafunzi hao kuanza kuripoti katika shule za sekondari, baadhi yao hawakuwa wamepata barua za kuwaalika shule walizoitwa.

Kulingana na Bw Charloz Okisai, mzazi kutoka Busia, mwanawe Josephat Seth Imai aliyepata alama 381, aliitwa katika shule ya kitaifa ya wasichana ya Kapsowar.

Hii ni baada ya Baraza la Kitaifa ya Mitihani (Knec), kumtambulisha kama msichana katiika cheti chake chake KCPE. “Kwa sababu ya makosa hayo, mwanafunzi huyo aliitwa kujiunga shule ya wasichana na juhudi za kuomba wizara kurekebisha makosa hayo zimegonga mwamba,” alilalamika mzazi huyo. Tukienda mitamboni jana, maafisa wa elimu wa kaunti walikuwa wakijaribu kumtafutia Imai nafasi katika shule ya wavulana ya Butula, Kaunti ya Busia.

Hali kama hiyo iliripotiwa katika Kaunti ya Nairobi ambapo mwanafunzi mvulana alikwama baada ya kupata barua ya kujiunga na shule ya wasichana.

Mamia ya wanafunzi waliofanya mtihani huo mwaka jana hawakuwa wamepata barua za kujiunga na shule za sekondari licha ya wizara ya Elimu kutangaza kuwa wataanza kuripoti Jumatatu Januari 7.

Wizara hiyo ililaumiwa kwa kuonya walimu wakuu dhidi ya kuwasajili wanafunzi moja kwa moja bila kupitia kwa wizara.

“Kuna wazazi ambao watoto wao waliitwa shule za kitaifa lakini hawawezi kumudu karo na wanataka kuwapeleka shule za karibu na nyumbani. Wizara inapasa kubatilisha agizo hili,” alisema Bw Njuguna Kawanjiku, diwani wa wadi ya Mweiga, Kaunti ya Nyeri.

Wazazi walilalamika kuwa agizo la serikali litaathiri wale masikini na wanaotaka kuhamisha wanafunzi wao kwa sababu za dharura.

Katibu wa tawi la Tharaka-Nithi la chama cha walimu (Knut), Njeru Mutani, alisema wazazi kutoka mashambani hupenda kupeleka watoto wao shule za karibu ambapo wanaweza kulipa karo kwa kutumia mazao au kufanya vibarua. Mbunge wa Imenti Kusini, Kathuri Murungi alikosoa wizara ya Elimu akisema ni kudhulumu wanafunzi waliokosa kuitwa shule walizokuwa wamechagua.

Maafisa wa vyama vya kutetea wanafunzi Kaunti ya Kisii walisema agizo la wizara linakiuka uhuru wa wanafunzi wa kujiunga na shule wanazopenda.

Naye katibu wa tawi la Busia la chama hicho, Mark Oseno alionya kuwa agizo hilo litaathiri wanafunzi ambao hawakupata barua za kujiunga na shule za upili licha ya kupata alama bora kwenye mtihani.

Na Faith Nyamai, Grace Gitau, Alex Njeru, Joseph Wangui, Irene Mugo, Derick Luvega, Ruth Mbula, Vivere Nandiemo, Gaitano Pessa, Rushdie Oudia, Gerald Bwisa, Oscar Kakai na Flora Koech.