Habari za Kitaifa

Presha ilivyolemea Serikali, ikalazimika kudondosha baadhi ya ushuru

Na JUSTUS OCHIENG’ na CHARLES WASONGA June 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

SERIKALI ya Rais William Ruto imelegeza kamba kutokana na presha kutoka kwa umma na kuondoa baadhi ya ushuru kadhaa dhalimu zilizopendekeza katika Mswada tata wa Fedha wa 2024.

Wabunge wa Kenya Kwanza Jumanne waliondoa aina za ushuru uliopendekezwa kutozwa mkate, magari, mafuta ya kupikia na mazao ya shambani huku nyongeza ya ushuru kwa huduma za kifedha ikisitishwa.

Mswada huo ulikuwa umependekeza mkate utozwe ushuru wa VAT wa asilimia 16, ushuru wa magari wa asilimia 2.5, ushuru wa asilimia 25 kwa mafuta ya kupikia, ushuru wa asilimia 16 kwa miwa inayowasilishwa viwandani na nyongeza kwa ushuru wa kutuma na kupokea fedha kwa njia ya simu kutoka asilimia 15 hadi asilimia 20.

Akihutubia kikao cha wanahabari baada ya mkutano wa kundi la wabunge (PG) katika Ikulu ya Nairobi, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah alisema, wameamua kufanya mageuzi hayo kwa mswada huo baada ya kusikia “kilio kutoka kwa Wakenya,”

“Sharti tuwakinge Wakenya kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha na ushuru wa VAT wa asilimia 16 uliopendekezwa kutozwa mkate umeondolewa. Ili kupunguza gharama ya maisha hata zaidi tumeondoa ushuru kwa mafuta ya kupikia na ushuru wa mazingira kwa bidhaa zinazotengenezwa nchini,” akaeleza.

Waandamanaji na wapita njia katika hali ya mguu niponye kufuatia mabakiliano na polisi kuhusu Mswada wa Fedha 2024. Picha|Evans Habil

Lakini Bw Ichung’wah na wabunge wa Kenya Kwanza walipokuwa wakitangaza afueni kuhusu ushuru kwenye Mswada huo, polisi walikabiliana na raia katika barabara za Nairobi walioshiriki maandamano ya kuupinga mswada huo.

“Vile vile, tumeondoa ushuru wa VAT wa asilimia 16 uliopendekezwa kutozwa usafirishaji miwa kutoka shambani hadi viwandani. Aidha, hakutakuwa na nyongeza ya ushuru unaotozwa huduma za kifedha na ubadilishanaji wa sarafu ya kigeni,” Bw Ichung’wah akawaambia wanahabari katika Ikulu ya Nairobi.

Pamoja naye walikuwa Rais Ruto, Naibu Rais Rigathi Gachagua, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, wabunge na maseneta wa muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha, Kuria Kimani alieleza kuwa wanachama wa kamati yake waliamua kupendekeza mabadiliko kwa mswada huo baada ya kusikiza maoni kutoka kwa umma na wadau wengine.

“Hii inaonyesha kuwa, vikao vya umma vilivyoendeshwa na kamati yangu kukusanya maoni kutoka kwa wadau na Wakenya vilikuwa na maana; havikuwa shughuli za uhusiano mwema,” akaeleza.

Bw Kimani pia alisema kamati yake pia iliweka mapendekezo yanayolinda wafanyabiashara wadogo.

“Tumependekeza kuongeza kiwango cha thamani ya biashara zitakazohitajika kujisajili kwa ushuru wa VAT kutoka Sh5 milioni hadi Sh8 milioni,” akaeleza.

“Isitoshe, agizo la Mamlaka ya Ushuru Kenya (KRA) kwamba wakulima na wafanyabiashara watumie mashine za ulipaji ushuru kieletroniki (ETIMS) limefutwa. Hii itatoa afueni kwa mama mboga ambao faida yao haitimu Sh1 milioni kwa mwaka,” Bw Kuria, ambaye ni mbunge wa Molo akaongeza.

Kuhusu ushuru wa mazingira, Bw Kuria alisema kuwa kamati yake iliamua kuondoa pendekezo la kutozwa kwa bidhaa zinazotengezwa nchini ili kulinda viwanda vya humu nchini.

Mwandamanaji huyu jasiri aonekana kutotishwa na vitoa machozi alivyorushiwa almradi awasilishe ujumbe wake. Picha|Evans Habil

“Kwa hivyo, bidhaa kama nepi, pikipiki, simu za mkono miongoni mwa zingine sasa hazitatozwa ushuru huu unaolenga kuzuia uchafuzi wa mazingira. Tumeamua kuwa ni bidhaa zinazoagizwa kutoka nje pekee ndizo zitatozwa ushuru huu,” akaeleza.

Kamati hiyo ya fedha pia iliondoa ushuru kwa mayai, vitunguu na viazi vinavyozalishwa nchini Kenya ili kuwafaa wakulima wa humu nchini.

Kuhusu michango ya pensheni, Bw Kimani alisema kuwa kamati yake imeongeza kiwango ambacho hakitatozwa ushuru kutoka Sh20,000 kwa mwezi hadi Sh30,000.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya wabunge wa Kenya Kwanza kutangaza mapendekezo hayo yanayolenga kutoa afueni kwa Wakenya, baadhi ya wabunge wa Azimio waliyapuuzilia mbali wakitaja kama “shughuli za uhusiano mwema”.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Amos Mwago (Starehe) na mwenzao wa Matungulu Stephen Mule walihoji mapendekezo ya kamati ya Bw Kimani wakisema hayatatoa ufueni kwa Wakenya wenye mapato ya chini.

“Asilimia 80 ya bidhaa zinazotumiwa nchini, vikiwemo vyakula huagizwa kutoka ng’ambo.

Kwa hivyo, gharama ya maisha itaendelea kuwa juu ikiwa bidhaa hizo zitatozwa ushuru wa mazingira wa asilimia 20,” Bw Owino aliwaambia wanahabari katika majengo ya bunge.