Habari Mseto

KURA yasitisha kwa muda ufurushaji wafanyabiashara wanaouzia kandokando mwa barabara


MAMLAKA ya Barabara za Mijini (KURA) imesimamisha kwa muda notisi ya kuwafurusha wafanyabiashara wanaouza kando ya barabara Wadi ya Nairobi South, Kaunti ya Nairobi.

Wiki chache zilizopita, KURA ilitoa notisi kwa wafanyabiashara wanaouza kando ya barabara katika wadi 17 Kaunti ya Nairobi kusitisha shughuli zao kwani uuzaji kandokando mwa barabara umepigwa marufuku.

Uamuzi huo wa kusitisha mpango huo umefikiwa baada ya diwani wa eneo hilo, Waithera Chege, kuzungumza na mamlaka hiyo na kukubaliana kutowafurusha wafanyabiashara hao zaidi ya 1,000.

Bi Chege alisisitiza kuwa hakukuwa na soko hata moja katika wadi hiyo ya Nairobi South, hivyo waliomba muda zaidi kuruhusu ujenzi wa soko linalotarajiwa kujengwa katika eneo hilo.

Bi Chege alisema, “Tumekubaliana na KURA kuwapa wafanyabiashara muda wa kuendelea na shughuli zao huku tukihakikisha usafi unazingatiwa na kuondoa uchafu wote ulioko katikati mwa barabara.”

Pia, Bi Chege aliahidi kuendelea kupambana na visa vya unyakuzi wa vipande vya ardhi ya umma katika Wadi ya Nairobi South, ambavyo vimekithiri mno katika eneo hilo.

“Nitaendelea kupambana na visa vya unyakuzi wa ardhi ya umma ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanapata maeneo salama ya kuendeleza shughuli zao.”