Habari Mseto

Kibagendi alivyojaribu kumwaibisha Sudi wakati wa upigaji kura Bungeni


KIOJA kilishuhudiwa bungeni Alhamisi pale Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Antony Kibagendi aliponyanyuka kwa hoja ya nidhamu akimjulisha Spika kuhusu kuwepo kwa “mtu tusiyemfahamu miongoni mwetu.”

“Mheshimiwa Spika kuna jamaa aliyeingia hapa na ambaye hatumfahamu. Jina lake ni Oscar Sudi na sina uhakika kama ni mmoja wetu,” akasema.

Spika Moses Wetang’ula alimrukia mbunge huyo, aliyechaguliwa kwa tiketi ya ODM, kwa maneno makali huku akimwonya dhidi ya kuibua mzaha bunge lilipokuwa lishughulikia suala muhimu kama Mswada wa Fedha 2024.

“Koma kabisa kuibua hoja za nidhamu zisizo za msingi wowote katika bunge. Sina wakati wa mzaha kama huo. Subiri zamu yako kuchangia mjadala kuhusu mswada huu badala ya kuibua mambo yasiyo na maana,” Bw Wetang’ula.

Bw Sudi, ambaye anahudumu muhula wa tatu kama Mbunge wa Kapseret, ni miongoni mwa wabunge ambao ni nadra kwao kuhudhuria vikao vya bunge.

Wao hufika bungeni tu wakati wanapohitajika na vyama vyao kupigia kura mswada au hoja fulani bungeni

Juzi, wakazi wa eneo bunge hilo walimponda kwenye mitandao ya kijamii wakidai ametelekeza majukumu yake bungeni.

“Tunamwambia Oscar Sudi hivi; umekubali kwamba huwa huhudhurii vikao vya bunge. Umekuwa ukifanya nini kwa miaka 12 iliyopita? Ujiuzulu ikiwa ni vigumu kwako kufanyia kazi watu wa Kapseret,” akasema Mary Chepkurui kupitia mtandao wa kijamii wa X.

Mkazi mwingine aliyejitambulisha kama Kogo alisema imewapambazukia kuwa walimchagua kiongozi ambaye hawezi kuwawakilisha ipasavyo katika Bunge la Kitaifa.

“Oscar Sudi, watu wa Kapseret walikupeleka bunge kuangazia matatizo yao. Ni aibu kukusikia ukiambia taifa kwamba hauwezi kuhudhuria vikao vya bunge kunywa chai. Kwani tulikosea kukuchagua kama kiongozi asiyeweza kutuwakilisha bungeni? Mbona unazunguka kote nchini ukiongoza michango ya harambee kusaidia wengine ilhali sisi tunaumia?” akauliza.

Mwezi jana, Bw Sudi ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais William Ruto, akinukuliwa akikiri kwamba yeye huwa hahudhurii vikao vya Bunge kwa sababu “huwa nimebanwa na shughuli za kusaka hela humu nchini na ng’ambo kusaidia wasiojiweza katika jamii.”