Habari za Kaunti

Kaunti zapokea dozi za dawa za watoto wachanga

Na ELIZABETH OJINA June 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

HOSPITALI za rufaa katika Kaunti za Kisumu, Homabay, Kisii, na Kakamega, zinatazamiwa kupokea dozi za kusaidia kudhibiti maradhi yanayodhuru watoto wachanga waliozaliwa kabla ya kufikisha miezi tisa.

Ufadhili huu kutoka kwa shirika la Clinton Health Access Initiative (CHAI) utapiga jeki pakubwa Afya ya watoto wachanga.

Unajumuisha takriban dozi 30,000 za caffeine citrate, dawa muhimu kwa matibabu ya muda mfupi kwa matatizo ya kupumua miongoni mwa watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati, maarufu kama Apnea of Prematurity (AOP).

Ufadhili huu umejiri baada ya wahudumu wa Afya kupokea matibabu ya siku tano kwenye Mpango Maalum wa Mafunzo Kutunza Watoto Wachanga.

AOP ni hali ambayo watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati hukumbwa na matatizo ya kupumua.

Hali hiyo huathiri watoto wachanga ambao mifumo yao ya pumzi bado haijakamilika.

Dozi ya caffeine citrate imeibuka kuwa tiba salama na mwafaka inayoboresha mchakato wa kupumua miongoni mwa watoto wachanga wanaoathirika kirahisi na kuwapunguzia tishio la kupata magonjwa sugu ya mapafu.

Hapo awali, dozi moja ya matibabu hayo ilikuwa ikilipishwa Sh 2,000, hivyo kuzidishia mzigo serikali za kaunti na kupunguza matumizi yake.

Mwelekezi wa Afya ya Watoto Kaunti ya Kisumu, Nicholas Pule, alisema ufadhili wa dawa hizo muhimu utaimarisha uwezo wa kutunza watoto wachanga waliozaliwa kabla ya kutimiza miezi tisa.

“Tumefurahi kutangaza kwamba, kupitia majadiliano bei ya caffeine imepunguzwa kwa asilimia 70. Hii ina maana kuwa dozi sasa itapatikana kwa Sh300, hivyo kuifanya tiba inayopatikana kirahisi,” alisema Mkurugenzi wa CHAI, Betty Wariari.

Tafiti zimeonyesha kuwa dawa ya caffeine citrate ina nguvu kupunguza makali ya matatizo ya maradhi ya kupumua kwa watoto wachanga, kuimarisha viwango vya hewa ya Oksijeni.