Mbunge ashauri wasichana wakome kuwapa ‘masponsa’ uroda
Na JADSON GICHANA
MBUNGE Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Kisii, Bi Janet Ong’era amewashauri wasichana wajiepushe kushiriki ngono na wazee wa rika la babu zao.
Alisema usuhuba katika ya wasichana wa vyuo na wazee unaendelea kikithiri katika maeneo ya Nyanza jambo ambalo huenda likasababisha ongezeko la maambukizi ya ugongwa wa Ukimwi.
Akizungumza na Taifa Leo mjini Kisii Bi Ong’era alisema mapenzi kama hayo mara nyingi huteka nyara fikira za wasichana hao kiasi kwamba hawana tena ile bidii ya kung’ang’ana katika maisha ili wafikie uthibiti wa kijamii na kiuchumi.
“Ningependa kuwatahadharisha wasichana wote. Jiepusheni na hii mipango ya kufadhiliwa kimapenzi na wazee matajiri. Utaishi vyema ndio ukionekana, lakini jua unajipotezea wakati wako muhimu wa maisha ya baadaye,” aliambia Taifa Leo.
Alieleza kuwa wanaume wengi huchukua hali yao ya umaskini kwa kuwashawishi na kuwadhulumu wasichana hao kwa kushiriki ngono.
Bi Ong’era pia alikemea visa vya unajisi vinavyozidi kuongezeka katika kaunti ya Kisii hivi karibuni.
“Ninawashauri wasichana wa umri mdogo kujiepusha na waze hao ambao nia yao ni kuharibu maisha na kutumia fursa ya gharama ya maisha ya familia ili kushiriki ngono na wao,” alisema Bi Ong’era.
Mbunge huyo wa Kaunti alisema kuwa baadhi ya hatari zilizoko ni kuambukizwa magonjwa kwa kuwa “sio wafadhili wengi wa kimapenzi watakubali kutumia kinga katika tendo la mapenzi.