Mpishi anayedaiwa kutishia kuua Ichung’wah kuhusu mswada wa fedha ashindwa kulipa Sh100,000
MPISHI aliyeshtakiwa Jumatano kutishia kumuua Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah endapo mswada wa Fedha 2024 utapitishwa ameshindwa kulipa dhamana ya pesa tasilimu Sh100,000.
Hivyo basi, Stephen Mwangi Kamau alimsihi Hakimu Mkazi Rose Ndubi ampunguzie dhamana hiyo hadi Sh50,000.
“Mheshimiwa siwezi kupata Sh100,000. Mimi ni mpishi katika hoteli moja jijini Nakuru. Mshahara wangu ni Sh6,500. Ijapokuwa Mungu anitendee muujiza siwezi pata pesa hizo,” Bw Kamau alimweleza hakimu Alhamisi.
Mpishi huyo alimweleza hakimu kwamba ndugu yake amefika mahakamani kutoka Nakuru na pesa zile familia imekusanya ni Sh15,000.
“Nimeoa na tumejaliwa watoto wawili. Pesa kidogo ninazopata ndizo tunatumia kujikimu kimaisha ndio maana mimi na Wakenya wengine tunapinga Mswada wa Fedha 2024. Hatuwezi kujimudu kamwe,” Bw Kamau alimweleza hakimu.
Mshtakiwa alieleza mahakama kwamba hata ingawa Rais William Ruto ameondoa Mswada huo “hali ni ngumu.”
Alimsihi hakimu ampunguzie dhamana angalau amfikishie Sh50,000 akitilia maanani hali yake ya uchochole.
Kamau anakabiliwa na mashtaka manne ya kutisha kumuua Bw Ichung’wah aliye pia Mbunge wa Kikuyu endapo Mswada wa Fedha 2024 utapitishwa.
Bunge liliupitisha mswada huo Jumanne na waandamanaji wakavamia majengo yake.
Ilikuwa ni hali ya mguu niponye kwa wabunge kuokoa maisha yao baada ya kupuuza maoni ya wengi wa wananchi.
Bw Ichung’wah alinunukuliwa akidai aliwaongoza wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza kupitisha mswada huo.
Mshtakiwa huyo alimweleza hakimu kwamba hali nchini inatokota na kwamba itabidi mahakama iingilie kati kuwatetea na kuwaokoa wananchi wa kawaida.
Bi Ndubi aliagiza mshtakiwa azuiliwe hadi Ijumaa atakapoamua ikiwa atampunguzia Kamau dhamana au la.
Kamau alikabiliwa na shtaka kwamba mnamo Juni 20,2024 mahala pasipojulikana humu nchini akitumia mtandao aliofungua kwa jina “Brand Trevor” uliosajiliwa kwa jina lake Stephen Mwangi Kamau, bila idhini alimtumia Bw Ichung’wah ujumbe wa vitisho katika mtandao wake wa WhatsApp.
Kwenye ujumbe huo mahakama ilifahamishwa Bw Kamau alimweleza bayana mwanasiasa huyo “Kimani naapa ikiwa mswada wa fedha 2024/2025 utapita, nitapanga jinsi utahusika katika ajali na kamwe hautapona.”
Hakimu alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka ya Umma kwamba mshtakiwa alimtumia ujumbe huo Bw Ichung’wah kwa mtandao wake wa WhatsApp @kimani Ichung’wah, alioandikisha katika kampuni ya Safaricom kwa jina Antony Kimani Ichung’wah.
Mbali na shtaka hili, Kamau amekabiliwa na mashtaka mengine mawili ya kumdhalilisha Bw Ichung’wah na Rais William Ruto katika jumbe alizomtuma Aprili 20,2024.
Shtaka lingine linadai Kamau alimpelekea Bw Ichung’wah ujumbe akidai ndiye anayewapiganisha Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.
Kamau alikana mashtaka manne dhidi yake na kuomba aachiliwe kwa dhamana.