Mdomo wamchongea Gachagua na kujipata motoni
NAIBU Rais Rigathi Gachagua amekosolewa vikali kwa kumshambulia Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Ujasusi (NIS) Noordin Haji na kumtaka ajiuzulu huku baadhi ya viongozi wakitaka mahakama iagize achunguzwe kwa uchochezi.
Mnamo Jumatano, Bw Gachagua alidai Bw Haji anafaa kuwajibika kwa vifo vilivyotokea wakati wa maandamano ya vijana akidai alikosa kumpa Rais habari sahihi za ujasusi.
“Haji lazima awajibike kwa vifo vilivyotokea na kwa ghasia na kwa kumfeli Rais Ruto na serikali na lazima awajibike kwa kufeli wananchi kwa kutofanya kazi yake na kutoa ushauri sahihi. Ni lazima afanye jambo la heshima, sio tu kuwajibika bali ajiuzulu kutoka afisi hiyo na kumruhusu Rais kuchagua Mkurugenzi Mkuu anayefaa,” Bw Gachagua alisema akihutubu akiwa Mombasa.
Kauli yake imeibua hisia kali kutoka kwa wazee wa jamii ya Wasomali, viongozi wa dini ya Kiislamu na wa upinzani.
Mnamo Alhamisi, Wazee wa jamii ya Wasomali kutoka Kaunti ya Garissa walimtetea Bw Haji dhidi ya madai ya Gachagua. Bw Dubat Ali Amey, mzee wa jamii, alisema inashangaza kwamba, Naibu Rais anaweza kutoa madai hayo hadharani.
“Kauli za Naibu Rais zilihusu kuchochea nchi na hazikuhitajika. Amedhamiria kuhakikisha kuwa serikali hii haifanikiwi,” Bw Amey alisema, na kuongeza kuwa ofisi ya Naibu Rais inapaswa kumsaidia Rais katika kuendesha serikali na wala si kupigana na mkubwa wake.
“Tunamwambia naibu rais amsaidie Rais katika kuunganisha nchi lakini sio kuigawanya kwa misingi ya kikabila,” alisema. Bw Amey alisema Bw Gachagua anashikilia afisi inayoheshimika lakini tabia yake inatia shaka.
Kulingana na Mzee Ali Shebe, Naibu Rais amekuwa na tatizo na Bw Haji tangu alipokuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa sababu ya kesi zake zilizokuwa mahakamani.
“Tunamtetea mtoto wetu anayeongoza NIS. Naibu Rais amesahau wajibu wake wa kumsaidia Rais kuhusu hali ilivyo sasa lakini badala yake anajihusisha na lawama,” akasema.
Wazee hao walisema Bw Haji ni mtu mwenye uadilifu na Bw Gachagua hafai kumchafulia jina kwa sababu ya maslahi yake ya kibinafsi au kulipiza kisasi.
Jana Ijumaa, Baraza la Kitaifa la Viongozi Waislamu (NAMLEF) lilimtaka Naibu Rais Rigathi Gachagua kuheshimu itifaki na kuacha kujitangaza kama kiongozi wa eneo la Mlima Kenya pekee.
Mwenyekiti wa NAMLEF, Abdullahi Abdi, alisema kuwa hatua ya Bw Gachagua kumpinga waziwazi Dkt Ruto hasa baada ya Rais kujibu madai ya vijana waliokuwa wakiandamana inaleta wasiwasi mkubwa.
“Alimshambulia Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Taifa ya Ujasusi, Noordin Mohammed Haji ambaye jukumu lake ni muhimu kwa usalama wa taifa letu. Angeweza kutumia njia zilizopo kuelezea masikitiko yake kwa mkubwa wake ambaye ni rais,” Bw Abdi alisema.
Bw Abdi aliwaomba Wakenya kuwa macho wasichochewe na wanasiasa kama Gachagua kuwagawanya kwa misingi ya kikabila.
Naye kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi alitaja kauli ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhusu kushindwa kwa Idara ya Kitaifa ya Ujasusi kuwa inayohatarisha usalama wa taifa.
“Bw Gachagua anafaa kuheshimu kiapo alichokula alipoapishwa na kuacha kuropokwa ili kufanikisha amani na utangamano,” akasema.
Wakati huo huo, Gachagua ameshtakiwa kufuatia matamshi yake dhidi ya Bw Haji.
Katika kesi iliyowasilishwa chini ya sheria za dharura na wakili Danstan Omari, mahakama kuu imeombwa iagize tume ya uuwiano na utangamano (NCIC) ichunguze matamshi hayo ya Bw Gachagua kwa lengo la kumfungulia mashtaka.
Ripoti za Manase Otsialo, Mumbi Wainaina, Victor Raballa na Richard Munguti