SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Mataifa ya Afrika yaombwa yakumbatie lugha hiyo ya kiasili
HUKU mataifa mbalimbali yakijiandaa kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani Jumapili, washikadau mbalimbali wametaka mataifa ya Afrika kuwa katika mstari wa kwanza kukumbatia lugha hiyo ambayo inazidi kupata umaarufu duniani.
Kiswahili ni lugha ambayo ilichipuka Afrika Mashariki, inazungumzwa na mataifa 14 ikiwemo Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Sudan Kusini, Somalia, Mozambique, Malawi, Zambia, Comoros, Oman na Yemen Mashariki ya kati.
Haya yakijiri mataifa husika yameombwa kuchukua mstari wa mbele kueneza na kukuza lugha hiyo kama ilivyolenga shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO), kuongeza wazungumzaji wa lugha hiyo ambayo sasa ni zaidi ya milioni 200.
Kwa sasa, mataifa ya kusini mwa Afrika kama vile Afrika Kusini, Botswana wameongeza Kiswahili katika mitaala yao ya elimu, na mataifa kama Namibia na mengine yakiwazia pia kukumbatia juhudi hizo.
Wakizungumza huko jijini Mombasa katika Kongamano la pili la Kimataifa la Tume ya Kiswahili Barani Afrika lilioandaliwa katika hoteli ya Sarova Whitesands, wito ulitolewa kwa washikadau kuwekeza katika lugha kupitia kutoa machapisho zaidi ya vitabu na nakala za lugha.
Walihoji kuwa kueneza amani kupitia lugha hiyo kwa mataifa huenda kungesaidia lugha hiyo kukua zaidi.
Kwa mujibu wa profesa Kimani Njogu kutoka kampuni ya mawasiliano ya Twaweza, hakukuwepo na fedha za kutosha katika kuwekeza kwenye machapisho ya Kiswahili ilhali jamii zilikuwa na maarifa mengi ya lugha husika.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili ikiwa Kiswahili, Elimu Na Wingilugha Katika Ufanikishaji wa Amani, washikadau hao walisema ipo haja ya kukikuza Kiswahili na kukitumia kueneza amani katika baadhi ya nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Ni wajibu tuvuke mipaka ya kitaaluma kwa kuishirikisha jamii ili kuboresha ujenzi wa viwanda na kilimo kupitia uimarishaji wa lugha ya Kiswahili kwani jamii haiwezi kuwa na utulivu wa kiuchumi bila amani,” alisema.
Waziri wa Jinsia Utamaduni na Turathi, Bi Aisha Jumwa ambaye alikuwa mgeni mkuu alisema kuwa, ili kuleta uelewa wa sheria na sera nchini ziandikwe katika lugha ya Kiswahili.
“Hili litawezesha watu kuelewa kwani Kiswahili kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni mia mbili duniani kwa hiyo lazima tujivunie,” alisema Waziri.
Pia tathmini ya mchango wa gazeti wa Taifa Leo la Kidijitali ulipigwa shime katika kueneza amani nchini Kenya kupitia mada, maoni au kauli na hata nukuu za watu wanaolenga kueneza amani.
Huko Lamu, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Bw Mohamed Shee Mbwana alisisitiza haja ya serikali kuibuka na sheria maalum itakayoshinikiza au kulazimisha wananchi kuongea Kiswahili, iwe ni maofisini, mabarazani na mitaani.
Bw Mbwana alielezea kutamaushwa kwake na jinsi wazungumzaji kwenye makongamano mbalimbali yanayoandaliwa nchini, ikiwemo yale ya Kiswahili hupendelea sana kutumia Kiingereza badala ya lugha tukufu ya Kiswahili.
“Twashukuru Kenya kwa kukiorodhesha Kiswahili kuwa lugha ya taifa. Ila hilo halitoshi. Tumejionea wazungumzaji wakikimbilia kutumia Kiingereza kwa wingi kuliko Kiswahili. Tungeomba serikali kuibuka na sheria ya kuwalazimisha wananchi kukizungumza na kukienzi Kiswahili hata ikiwa ni kwa siku moja pekee kila wiki. Tukifanya hivyo ninaamini hadhi ya Kiswahili itaheshimiwa na kutambuliwa zaidi,” akasema Bw Mbwana.
Kilele cha siku ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani yatakolea siku ya Jumapili ambapo shamrashamra zimeandaliwa hasa kukikuza na kukivunia Kiswahili kama lugha ya Taifa Nchini.
RIPOTI ZA Jurgen Nambeka, Fatma Bugu na Kalume Kazungu