Dimba

Mambo ni manne! Kibarua cha Ten Hag baada ya dili mpya kambini Man Utd

Na CHRIS ADUNGO July 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BAADA ya kutia saini mkataba wa miaka miwili, Kocha wa Manchester United Erik Ten Hag sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuboresha matokeo ya timu hiyo msimu ujao wa 2024-25.

Ten Hag alipokezwa mikoba ya kunoa Man United hadi 2026 baada ya wamiliki wa klabu hiyo kufuta mpango wa kumtimua mwezi uliopita.

Kocha huyo raia wa Uholanzi baada ya kuongezwa mkataba wiki hii alisema kuwa kuna kazi ngumu ya kufanya kurejesha Man United katika hadhi yake ya zamani.

“Lazima sasa tupambane ili kuwania mataji na kurejesha klabu hii katika hadhi yake ya zamani,” akasema Ten Hag, 54.

Kile ambacho kilimwokoa Ten Hag ni ushindi wa 2-1 ambao walipata Manchester City katika fainali ya Kombe la FA na kutwaa taji hilo.

Msimu wa 2022-23 alishindia United Kombe la EFL ambalo lilitwaliwa mara ya mwisho kocha wa zamani Sir Alex Ferguson akiwa usukani.

Ili kufufua timu hiyo, kibarua cha Ten Hag kitakuwa ni kuimarisha safu yake ya nyuma ambayo ilivuja sana msimu uliopita.

Pia itabidi klabu hiyo imsajili mchezaji nyota kuhimili safu ya kiungo cha kati, sehemu ambayo ilikuwa na tatizo sana.

Aidha Ten Hag lazima ahakikishe kuwa Marcus Rashford na Anthony wanaimarisha kiwango chao ili kusakia klabu hiyo magoli mengi.

Msimu jana wawili hao walishtumiwa kwa kuonyesha kiwango cha chini cha mchezo.

Rashford, raia wa Uingereza, alifunga mabao 17 pekee katika mechi 35 za EPL.

Ten Hag lazima amtumie vyema Rasmus Hojlund kuyapata magoli zaidi msimu ujao.

Raia huyo wa Denmark ni kati ya wanasoka ambao wamesazwa na uongozi wa klabu shoka lilipokuwa likiteremshiwa wanasoka wenzake.