Ichung’wah, wandani wake motoni kwa kuunga mswada
IWAPO Mswada wa Fedha wa 2024 ungetiwa saini na Rais William Ruto, basi Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah angeongeza ushawishi wake ndani ya serikali kuu.
Kinaya ni kuwa Bw Ichung’wah ambaye ni mbunge wa Kikuyu angechukiwa sana na wapigakura kutoka Mlima Kenya na eneo la Kiambu ambapo ana ubabe mkali wa kisiasa dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Baada ya Rais kukataa kutia mswada huo, baadhi ya wapigakura hasa katika Kaunti ya Kiambu wameapa kuwa hawatamuunga mkono siasa za Bw Ichung’wah kwa sababu aliwasaliti.
“Ichung’wah na wandani wake walikuwa wakifikiria kuwa wao ndio sauti ya Rais kuhusu siasa za Kiambu lakini sasa mambo ni tofauti. Nimefurahi kwa sasa wanafahamu wananchi ndio wasema kweli kuhusu suala lolote lile,” akasema muuzaji matunda kutoka Kikuyu Peter Nduati.
Baadhi ya wandani wa Bw Ichung’wah katika kaunti hiyo ni mbunge wa Thika Mjini Alice Ng’ang’a, George Kagombe wa Gatundu Kusini na Mbunge Mwakilishi wa Kiambu Anne Wamuratha ambao wote walipiga kura ya kuunga mswada huo.
“Alice alitusaliti kama wapigakura wa Thika kwa kuunga mkono mswada huo. Mungu ametufungua macho kama wapigakura na sasa tunafahamu kuwa hatuna wawakilishi bali watu ambao ni wafanyabiashara na wana ubinafsi,” akasema Mary Wanjiku, mfanyabiashara Thika Mjini.
Raia Geoffrey Kamau, kutoka Kirigiti ni kati ya wale ambao walimpigia Bi Wamuratha kura lakini sasa hataki kusikia chochote kuhusu kiongozi huyo.
Margaret Waithera kutoka Gatundu Kusini naye anasema alikuwa na matumani kuwa Bw Kagombe angewatetea raia kutokana na sifa zake za uanaharakati lakini akashangaa alipigia kura mswada huo katili.
“Nilimpigia kura Kagombe na nakwambia najuta kufanya hivyo. Hawa wanasiasa huabudu tu wale ambao wanawalisha na si raia ambao waliwachagua,” akasema Bi Waithera.
Katika Kaunti ya Kiambu ni mbunge wa Juja George Koimburi na mwenzake wa Githunguri Gathoni Wamuchomba ndio walipinga mswada huo. Wawili hao ni wandani wa Naibu Rais Rigathi Gachagua.