Mjane kuhukumiwa kwa kuibia jamaa aliye na upungufu wa akili Sh467,000
MJANE mwenye umri wa miaka 53 amepatikana na hatia ya kuiba zaidi ya Sh400,000 kutoka kwa akaunti ya benki ya mwanaume anayeugua maradhi ya akili.
Hakimu mkuu Mahakama ya Milimani, Lucas Onyina alimpata na hatia Petronilla Kitony ya kuiba Sh467, 000 kutoka kwa akaunti ya Peter Kamau ambaye madaktari walisema alikuwa “anaugua maradhi ya dementia (mapungufu ya ubongo ya kutopambanua chochote na kusahau).”
Bw Onyina alisema Petronilla alikamatwa aliporudi katika Benki ya Family, ndiyo Family Bank (FBL) kuchomoa Sh968,000.
Kitumbua cha Petronilla kiliingia mchanga alipoombwa na mhudumu wa Benki ya FBL tawi la Donholm, Damarisa Nzisa asubiri hundi aliyopeana iidhinishwe na maafisa katika makao makuu.
“Mshtakiwa alitiwa nguvuni alipoenda kuiba Sh968,000 kutoka kwa akaunti ya Peter Kamau ambaye alikuwa amethibitishwa na madaktari hawezi kujielewa na wala hajui anachofanya kutokana na ugonjwa wa Dementia,” Bw Onyina alisema.
Hakimu alisema mshtakiwa alionyeshwa mahala pa kusubiri ndipo makao makuu ya FBL yakathibitisha “hakuna mtu yeyote aliyeruhusiwa kuweka pesa au kutoa pesa katika akaunti ya Peter Kamau kutokana na changamoto za ubongo wake.”
Mahakama ilisema mshtakiwa alikamatwa kama jinsi ndege hukamatwa ndani ya kiota na kufululizwa hadi afisi za maafisa wa kuchunguza makossa ya jinai katika Benki (BFU).
Hakimu alisema polisi walikuwa wameomba Benki za FBL na Equity (EBL) zisiruhusu mtu yeyote kuondoa au kuweka pesa katika akaunti za Peter Kamau aliyekuwa na changamoto za ubongo.
Mahakama ilisema uchunguzi ulibaini Petronilla alipokea Sh467,000 kutoka kwa akaunti ya Peter Kamau katika tawi la FBL Ruiru 2023.
Mahakama ilisema mshtakiwa alidai kitita cha kwanza alichochukua kilikuwa cha mfanyabiashara aliyekuwa ametoa huduma kwa serikali.
Akijitetea, mshtakiwa alisema aliandikiwa hundi hizo ili ajilipe pesa alizokuwa amemkopesha mfanyabiashara huyo aliyekuwa amepata zabuni kuuzia serikali bidhaa.
Lakini hakimu alitupilia mbali tetesi za mshtakiwa akisema “ni uzushi tu usiofua dafu.”
Akijitetea mshtakiwa alisema yeye ni mjane ambaye ni mama wa watoto watatu wanaomtegemea.
Petronilla alisema anaugua maradhi hatari na kwamba “anastahili chakula maalum.”
Hakimu aliamuru ripoti kuhusu mshtakiwa iwasilishwe ibainike ikiwa anahusika na ufisadi mwingine.
Bw Onyina atapitisha hukumu mnamo Julai 16, 2024 baada ya kupokea ripoti hiyo.