Juhudi za wanajeshi kupindua serikali Gabon zaambulia pakavu
MASHIRIKA na PETER MBURU
WANAJESHI nchini Gabon Jumatatu asubuhi walijaribu kupindua serikali ya nchi hiyo walipoingia kwa nguvu katika kituo cha redio ya serikali na kutangaza kuhusu namna hawajafurahishwa na Rais wan chi hiyo Ali Bongo.
Hata hivyo, serikali ya nchi hiyo ilitangaza kuwa saa chache baadaye, baadhi yao walitiwa nguvuni.
Msemaji wa serikali Guy-Bertrand Mapangou alieleza mashirika kuwa wanne kati ya wanajeshi watano ambao waliteka nyara kituo cha redio cha serikali walikamatwa, japo mmoja ambaye yuko mbioni anazidi kusakwa.
Afisa wa kijeshi ambaye hakukamatwa anasemekana kuwa kiongozi wa mpango huo wa kugeuza serikali ya Rais Bongo, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka mingi.
Nje ya kituo hicho cha redio, wanajeshi wengine walikuwa wakirusha gesi za kutoa machozi kutawanza takriban watu 300 ambao walikuwa wamejitokeza kuunga mkono mapinduzi hayo, mtu aliyeshuhudia akasema.
Katika ujumbe wa redio saa kumi na nusu asubuhi, Lieutenant Kelly Ondo Obiang ambaye alijitaja kuwa afisa katika kikosi cha Republican Guard alisema kuwa ujumbe wa Rais Bongo siku moja kabla ya mwaka mpya alipokuwa Morocco ambapo anapokea matibabu “ulizidisha hofu kuhusu uwezo wa Rais kuendelea kutekeleza majukumu ya ofisi yake.”
Hotuba ya Rais huyo ilikuwa hafifu na alionekana kutoweza kusongesha mkono wake wa kulia. Haijulikani ikiwa bado anatembea.
Rais huyo aliye na miaka 59 alipelekwa hospitalini mnamo Oktoba nchini Saudi Arabia baada ya kupooza. Tangu Novemba, amekuwa Morocco ambapo amekuwa akipokea matibabu.
Familia ya Bongo imetawala nchi hiyo yenye ukwasi wa mafuta kwa takriban miaka 50, kwani alipokea mamlaka kutoka kwa babake, Omar aliyeaga dunia mnamo 2009.
Uchaguzi wa Urais mnamo 2016 ulizingirwa na madai ya kura kuibiwa, maandamano ya fujo yakifuata.
Miaka ya majuzi, kumekuwa na upungufu mkubwa wa kiwango cha mafuta ambacho taifa hilo linatoa, pamoja na kiwango cha mapato kupungua vikubwa.
Katika video inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii, Ondo akivalia sare za kijeshi anaonekana akisoma ujumbe uliosomwa, ndani ya kituo hicho cha redio. Wanajeshi wengine wawili wanasimama nyuma yake wakiwa wamejihami kwa bunduki.
Afisa huyo alisema kuwa jaribio hilo la mapinduzi lilitekelezwa na kwa uongozi wa afisa wa ngazi ya juu katika jeshi, lakini akasema vikosi vingine vilikuwa vikifuatilia.
Bongo pamoja na maafisa wengine wa serikali yake wamekuwa wakikumbana na madai ya ufisadi na ulanguzi wa mali ya umma na serikali za nje, japo wamekana madai hayo.
Alishinda uchaguzi wa 2016 kwa chini ya kura 6,000, jambo lililopelekea machafuko kati ya waandamanaji na polisi na bunge la nchi hiyo kuteketezwa.